ROMA: Mwanaharakati mwanamuziki msomi


Historia yake
Ibrahimu Mussa ni kijana aliyezaliwa mkoani Tanga akiwa mtoto wa mwisho kati ya watoto watano katika familia ya kiislamu. Kwa sasa ni maarufu kama msanii R.O.M.A wa muziki wa kizazi kipya nchini Tanzania. Sehemu kubwa ya umaarufu wa Roma ni kutokana na nyimbo zake zenye maudhuu ya kuikosoa serikali kwa kile anachoona kina walakini na hiyo kumfanya mwanaharakati. Jina hili R.O.M.A kulingana nay eye mwenyewe ni muunganiko wa majina ya ndugu zake aliozaliwa nao pamoja, yaani Rashid, Omari, Maimuna, na Asha. Pia jina lake lina maana ya Rhymes of Magic Atraction (Mistari yenye  mvuto wa kichawi). Tarehe 12. 9. 2002 Roma alipata simanzi ya kumpoteza baba yake mzazi kutokana na maradhi ya muda mrefu.
Baada ya kifo cha baba yake Roma alizama zaidi katika mchezo wa kikapu aliokuwa anaupenda, ambao amekua akicheza tangu akiwa mdogo, ili tu kupunguza majonzi aliyokuwa nayo moyoni, na kipaji hiki ni moja ya mambo ambayo Roma hupendelea kufanya anapokuwa nje ya muziki kwani kwa sasa ni kocha wa timu aliyoichezea miaka ya 2000 za awali.
Aliingia rasmi kwenye tasnia ya muziki mwaka 2006 akiwa kidato cha sita mkoani Tanga. Lakini alianza kufahamika katika masikio ya watanzania mwaka 2008 alipoimba wimbo ulioitwa Tanzania na kugusa hisia za Watanzania wengi kutokana na kugusia changamoto zilizopo serikalini na kuikosoa serikali katika mistari ya wimbo huu.

Elimu.
Baada ya kumaliza elimu yake ya msingi, Roma alikwenda kusoma shule ya sekondari Usagara kwa miaka mine ni kasha kuchaguliwa kwenda shule ya sekondari Old Moshi, na hapo uanaharakati uliokua ndani yake ukadhihirika baada ya yeye na baadhi ya marafiki zake kufukuzwa shule kutokana na kusimamia misimamo yao ambayo haikuendana na matakwa ya shule.
Kutokana na tukio hilo ilimbidi kurudi shule ya sekondari Usagara aliposomea miaka mine ya awali na akaendelea na masomo yake hadi alipomaliza elimu ya sekondari.
Hapa ndipo kwa mara ya kwanza alipata nafasi ya kuonana na mtangazaji wa kituo cha Clouds FM, Hamis Mandi maarufu kama B’12. B12 alikua amekuja kwenye tamasha mjini Tanga na alikua anajiandaa kuondoka wakati ambapo Roma alitoroka shuleni ili kumpelekea cd yenye wimbo wake ulioitwa salute na akafanikiwa kuonana nae ndani ya basi likiwa limeshaondoka na baada ya kumkabidhi cd yake alishukia mbali na alipokua anasoma lakini yote hiyo ni ili aweze kutimiza ndoto zake. Alipomaliza shule ya sekondari alikwenda kufundisha shule ya sekondari ya Manza High. Pia  Ibrahim Mussa ni msomi mwenye shahada ya sayansi katika kompyuta.

Safari ya muziki
Roma anayejulikana kwa uvaaji wa rozali anasema mwaka 2007 ndipo aliamua kufanya muziki baada ya kuvutiwa na Profesa J.
Ambapo alirekodi wimbo wake wa kwanza uitwao Salute katika studio ya Mr Ebo iliyofahamika kama motika records, wimbo ambao ulifanya vizuri katika stesheni za redio za mkoani Tanga
Mwaka 2008 alitoa wimbo uliojulikana kama Tanzania, wimbo uliomuweka kwenye ramani ya muziki Tanzania, baada ya msimamo wake kuwa wazi kwa watanzania, nyimbo zake zilizofuata kama vile President, na Viva zilifanya vizuri kiasi cha kuligusa baraza la sanaa Tanzania.
Anasema wimbo wake uitwao Pastor, ndio uliompa matatizo zaidi baada ya kuonekana umekaa kidini na kupendelea zaidi dhehebu la Roman Catholic kutokana na mstari unaosema, “Zitakuja dini zote lakini RC itabaki.”

Radio nyingi ziligoma kuucheza wimbo huo na hivyo kudumu kwa miezi minne pekee.

Wimbo Mathematics ndio uliompa umaarufu maradufu baada ya kumpa tuzo mbili za Kili, mwanamuziki bora wa Hip hop wa mwaka 2011 na wimbo bora wa Hip Hop wa mwaka 2011.
Mambo ya kujifunza
1. Roma alikuwa na ndoto za kucheza mpira wa kikapu katika daraja la kulipwa, alikua na ndoto ya kua rubani, ndoto za kuwa mwanamuziki na ndoto nyingi sana tangu akiwa mdogo, lakini aliishia kufanya kile alichopenda zaidi, yaani kuimba. Ni vyema kufanya kitu kile unachofurahia kufanya ili kikuingizie kipato, badala ya kufanya kazi ambayo kila siku ukiamka unatamani ungekuwa ukifanya kitu kingine.
2. Roma amekua mwanaharakati ambaye anaikosoa serikali na hivyo kuhusishwa na chama cha upinzani cha chadema. Hali ambayo imewagawa mashabiki wake na kupunguza ufanisi wa kuifikia hadhira yake. Mara nyingi ni vyema kutojihusisha wazi na siasa endapo unapenda kuifikia hadhira kubwa au wateja wengi kwani kuna watu watakuchukia kwa sababu tu wewe ni chama Fulani. Ni vyema kufanya itikadi za vyama kuwa ni jambo la binafsi.
3. Pamoja na kukosa malezi ya baba katika wakati ambao ni mgumu katika maisha yake, Ibrahimu Mussa hakuacha shule, pamoja na kuwa na kipaji na kujiamini katika kile alichokua anafanya bado alienda akasomea masomo ya sayansi ya kompyuta ambayo yanaweza kuwa msaada mkubwa sana kwake pale atakapoamua kufanya shughuli tofauti na kile anachofanya sasa hivi. Hali hii inampatia upeo mpana wa uchaguzi wa ni wapi aweke mirija yake ya kutafuta fedha.
4. Roma anafahamika kama mtu wa watu, nyumbani kwao Tanga, Dar es salaam na Tanzania kwa ujumla ndio maana kampeni kubwa imefanyika nchi nzima ya kutafuta kufahamu ni wapi alipo Ibrahim Mussa. Baada ya kupata mafanikio Fulani katika muziki hakuwasahaau wale aliocheza nao na kujifanya kama hawajui, alirudi na akawa kocha wa timu aliyokua anachezea ili kuonyesha uzalendo.
5. Pamoja na kujihusisha na muziki, pi Roma ni baba wa familia yenye mtoto mmoja na ni mjasiriamali anayewekeza kile anachopata kutoka kwenye muziki. Uwekezaji ndio siri ya utajiri, uwekezaji ndio umemfanya AY kuwa mwanamuziki tajiri, uwekezaji ndio umemfanya Masanja Mkandamizaji kuwa mchekeshaji, mhubiri, na mjasiriamali tajiri pamoja na vioo wengine wengi wa jamii.
6. Roma ni moja kati ya wasanii ambao hawatumii madawa ya kulevya, hali hii imemfanya kutilia mkazo vipaumbele na malengo yake na kumfanya kufanikiwa kimuziki na katika ujasiriamali kwa kipindi cha takribani miaka kumi tu tangu alipomaliza shule ya sekondari. Madawa ya kulevya huathiri sana vijana wengi ambao wangeweza kuleta tofauti kubwa sana katika jamii ya watanzania, kuna mifano kama Chid benz, Tid, squeezer na wengine ambao wamepotea katika tasnia hii kwa sababu ya kujihusisha na madawa ya kulevya.
Kosa lake
Kuna nadharia nyingi zinazozungumzia kutekwa kwa Roma, kila mtu ana nadharia yake lakini ukweli hata Roma mwenyewe anaweza asifahamu. Mimi naweza nikasema kwamba suala zima la kutekwa kwa Bwana Ibrahimu Mussa sio za kimuziki bali ni kutokana na harakati za maisha yake binafsi kwani unapokuwa mtu maarufu unajihusisha na watu wa aina nyingi na hii hujenga maadui ambao wanakuwa tayari kukutumia katika kutimiza azma waliyo nayo, inaweza ikawa kuwasaidia katika biashara Fulani haramu, au kubadilisha mwelekeo wa vyombo vya habari kutoka kwenye habari Fulani iliyogusa usikivu wa watanzania na sasa inapaswa kuzimishwa, au inaweza ikawa ni chuki binafsi. Lakini hata polisi wafanye uchunguzi gani ukweli utabaki kati ya wachache, labda kati ya wachache hao atokee msaliti.
Hitimisho
Ibrahimu Mussa anasimama kama mfano wa kijana mwanaharakati anayetumia kipaji chake kufikisha dukuduku zake kwa jamii na kulipwa wakati akifanya hivyo, ni mfano mzuri kwa vijana wanaotamani kuingia katika tasnia ya muziki na wanaacha shule wakidhani safari ya kugonga milango ya vituo vya habari ni rahisi kwani yeye mwenyewe alibezwa alikataliwa na alisubiri mwaka mzima kabla hajapata nafasi ya kusikika katika kituo kikubwa cha redio, hivyo ni vyema kupata elimu ya darasani, lakini ni vyema zaidi kufanyia kazi kile unachokipenda na kile unachokiweza zaidi ili kikuingizie kipato. Katika ulimwengu wa sasa ni vyema kuwa na elimu na kipaji na kuvichanganya pamoja kuleta muunganiko utakaokuingizia fedha. Unaweza ukawa daktari lakini mchoraji, unaweza ukawa mkandarasi lakini mbunifu wa mitindo, unaweza ukawa mwalimu na ukawa mjasiriamali, unaweza ukawa mtangazaji wa kituo cha habari na ukawa blogger, unaweza ukawa fundi wa magari lakini ukawa mwimbaji. Popote ulipo muunganiko huo utaweza kukupatia upeo wa kufika mbali.


Na mkereketwa.

Comments

Popular Posts