Kilimo na Ufugaji sehemu ya pili/ Biashara ya Ufugaji wa Kuku wa Kienyeji

Awali ya yote ningependa kuomba radhi kwa kushindwa kuwakilisha makala hii kwa muda uliopangwa kutokana na kuharibika kwa kifaa changu cha  kazi. Ninashukuru kupata nafasi ya kushirikiana nanyi tena mambo machache katika makala hii.

Ufugaji ni sekta yenye faida nyingi kwa watanzania. Baadhi ya watanzania wamejihusisha katika ufugaji na kupata mafanikio makubwa. Sekta hii inaweza ikatumika katika kukuza mtaji, au katika kuleta mtiririko wa fedha.
Kuna aina nyingi za ufugaji kutegemea na mtaji wa mfugaji na aina ya wanyama anaofuga. Kuna aina nyingi za wanyama na ndege wanaofugwa kwa ajili ya biashara, baadhi yao ni ng’ombe, mbuzi, kondoo, kuku, kanga, batamzinga, kanga, kware, njiwa, sungura, nk. Ambao hutumika kwaajili ya matumizi ya nyama, au bidhaa za wanyama hao mfano maziwa na mayai.
Katika makala hii tutajikita katika ufugaji wa kuku wa kienyeji kwa ajili ya biashara, ungana nami ninapokuletea muendelezo wa makala iliyopita ikiwa ni mtiririko wa makala za biashara ya kilimo na ufugaji.
Kuna aina nyingi za kuku ambazo zinaunda makundi matatu ya kuku ambayo ni kuku wa kienyeji, kuku wa kisasa wa nyama na kuku wa mayai. Kama nilivyosema hapo awali kwamba katika makala hii tutakuwa tukiangalia ufugaji wa kuku wa kienyeji. Hivyo nitaanza kwa kukupatia aina za kuku wa kienyeji. Kwa sehemu kubwa kuku hawa wanatambulika kwa muonekano wao;
1. Kishingo - kuku wasio na manyoya shingoni

2. Njachama au Nungunungu - Hawa ni wale wenye manyoya yaliyosimama.

3. Kibwenzi - Ni wale wenye manyoya mengi kichwani.

4. Kibutu- Hawa hawana manyoya mkiani

5.     Kuroiler

6. Hybrid/  Chotara - Mwingiliano wa vizazi unaweza ukasababisha kuku kuwa na aina ya maumbile mchanganyiko. Mfano kuku aina ya kuchi anaweza kuwa na alama ya kishingo, Njachama, Kibwenzi au Kibutu.


JINSI YA KUFUGA KUKU WATANO HADI UPATE KUKU MIA MBILI
Anza na kuku Watano (5) tu Majike wenye Rika/Umri mmoja (au wanaokaribiana). Watunze vizuri kwa kuwapatia chakula kilicho na mchanganyiko kamili wa viini lishe vinavyotakiwa katika mwili wa kuku, yaani; wanga, protini, calcium, chumvichumvi, madini joto nk (kama nilivyoeleza hapa chini). Wawekee na Jogoo mmoja mzuri wa kienyeji/kizungu/chotara (kama nilivyoeleza hapa chini juu ya uchaguzi wa majogoo).

Wanapoanza kutaga watayarishie mahali pazuri/Kiota kizuri cha kutagia na kuatamia kwa kuwajengea viota ndani ya banda. Hakikisha mahali hapo hapavuji wala hapapati unyevunyevu wala joto kali sana. Hakikisha mahali hapo pana usalama wa kutosha (mahali wanyama hatari kama vicheche, pakashume, nyoka nk hawawezi kufika).

Kuku wakiendelea kutaga na sasa ukaona wanakaribia kuatamia,Anza kuchagua aina ya mayai unayotaka kuku wako walalie. Hii inamaanisha kuwa; ukichagua mayai makubwamakubwa hayo yanakuwa na vifaranga majogoo na mayai madogomadogo mara nyingi huwa ni ya vifaranga majike. Acha kuwawekea mayai ya mviringo kama mpira!

Hakikisha kuku wote wanasubiriana ili walalie/waatamie kwa pamoja.

Weka mayai 12 hadi 15 kwa kila kiota cha kuku 1 kulingana na umbo la kuku wako. Kuku anaweza kutaga hadi mayai 30 kwa kila msimu wa kutaga unapofika. Unaweza kutumia mayai machache kati ya 30 kwa kumuatamishia kuku wako huku mayai mengine yakisubiri awamu ya pili ya kuatamiwa.Kwa mfano ukiwawekea kuku wako hao watano, Kuku 5 x Mayai 12 = Mayai 60.

Kwa kawaida kuku huatamia/hulalia mayai kwa siku 19 hadi 21/24 tu hadi anapototoa vifaranga. Hakikisha unawawekea kuku walioatamia chakula chenye viini lishe vya kutosha na maji mengi karibu na viota vyao ili wakitoka kwenye viota vyao wale chakula mara moja na kunywa maji kisha warudi haraka kwenye mayai yao. Hii itasaidia kuangua mayai yote 12/15 bila kuharibu yai hata moja. Au hata yakiharikbika basi hayataharibika mengi kama ukiacha kuwawekea chakula waende kufukuzana na panzi na vyakula majalalani huko nje na kuchelewa kurudi kwenye mayai yao.

Wakati ukisubiria siku hizo 21/24 anza kujenga kibanda kidogo ndani ya banda kubwa ulilojenga awali au jikoni au andaa boksi kubwa na gumu kwaajili ya kutunzia vifaranga watakaoanguliwa ndani ya siku 21/24 zijazo.

Baada ya kuku hao 5 kuangua vifaranga wako 60 hapo ndipo kazi kubwa ya kulea vifaranga inapoanza. Elewa kuwa ili upate mafanikio haraka hakikisha kuwa kazi ya kulea vifaranga inakuwa yako na siyo ya kuku! Kwanza, Unatakiwa kuondoa na kuchoma moto/kufukia mabaki yote ya mayai na kuboresha usafi wa banda lote ili kuepusha magonjwa kama vile kuharisha, viroboto, papasi nk. Hapo unaweza kuwatoa vifaranga wako wote 60 mmojammoja kadri wanavyoanguliwa hadi kufikia kifaranga wa mwisho, yaani Yule wa 60 na kuwaweka katika kibanda kidogo/boksi ulichokijenga na kuwawekea mayai mengine mama zao (yale 15/18 kati ya 30 uliyoyabakiza) ili waatamie tena kwa siku 21 hadi 24 zingine. Unapotoa kifaranga kutoka kwa kuku aliyeatamia humfanya kuku Yule ashindwe kutoka kwenye mayai maana hana mtoto wa kulea.

Akimaliza kuangua mayai yote na ukamuwekea mengine ni rahisi kwake kuendelea kuatamia maana atasubiri kupata vifaranga na ndipo atajikuta amelalia kwa siku 21 zingine bila wasiwasi. Kwa kufanya hivyo utakuwa tayari umejipatia vifaranga/kuku zaidi ya 100 ndani ya wiki 7 tu! Sasa Unatakiwa kuwajali sana kuku hawa wanaolalia kwa mara ya pili kwa kuwapa chakula cha kutosha, maji, majani ya makongwe, mchicha, mchunga nk ili wapate vitamini na madini mengine muhimu kwa afya zao. Fanya hivyo hata watakapokuwa wametotoa na ukawanyang'anya vifaranga. Hii itawasaidia ili wasinyonyoke sana manyoya maana kuku wengi hunyonyoka manyoya wanapoatamia. Kwa kufanya hivi, kuku wako watakaa kwa wiki 2 hadi 3 bila vifaranga na kisha wataanza kutaga tena na kuatamia kama mwanzo.

Vifaranga wako hakikisha unawatengenezea chumba chao kido ndani ya banda kubwa/jikoni, kisha wawekee chanzo chochote cha joto kama vile; taa ya chemli/jiko la mkaa/vizinga vya moto nk ili wasiathiriwe na baridi hasa wakati wa usiku. Umakini mkubwa sana unatakiwa hapa! Hakikisha unakuwa makini wakati wa usiku ili kuongeza na kupunguza joto ndani ya kibanda cha vifaranga maana wakati huu maranyingi joto hupungua na ubaridi huongezeka na hivyo unaweza kuua vifaranga wako.

NAMNA YA KULEA VIFARANGA.

Katika ulezi wa vifaranga kama kuku utawanyang'anya vifaranga vyao utatakiwa kuwajengea banda dogo (ndani ya banda kubwa/uzio) ili uwawekee chanzo cha joto kama taa/jiko la mkaa (kama ni sehemu/majira ya baridi). Kama utatumia jiko la mkaa unatakiwa kuacha kwanza hadi mkaa mweusi uwake wote ndipo uweke bandani maana mkaa ukitoa moshi unaweza kuathiri vifaranga vyako. Angalia namna ya kuweka jiko lako la mkaa juu kidogo ili vifaranga wasiungue. Hakikisha taa yako haitoi moshi sana na haivujishi mafuta. Pia uwe na akiba ya mafuta ya taa ya kutosha. Usiweke mafuta mengi kwenye taa maana inaweza kulipuka ikakuletea hasara. Vifaranga wasizidi 50 kwa boksi 1. Hakikisha umewasha taa/jiko lako ndani ya boksi saa tatu au zaidi kabla ya kuwaweka vifaranga ili chumba/boksi lipate joto kabla ya vifaranga kuwasili. Njia hizi zinahitaji uangalifu wa hali ya juu sana kwani kuhatarisha/kuua vifaranga ni kuhatarisha maendeleo yako. Kama utaamua kutumia umeme pia ni vizuri zaidi maana inapunguza hatari zaidi.
Baada ya wiki ya 4/5 pasua box/watoe kwenye banda la kulelea ili walelewe kwa joto la kawaida la banda/chumba.
Kwa kawaida joto hupimwa kwa kipimajoto (thermometer), lakini kama huna kipimo hiki, njia rahisi ni kuwaangalia kulingana na tabia zifuatazo; Kama vifaranga wamejikusanya sehemu moja basi joto ni kidogo bandani mwao, au kama wanaenda mbali na chanzo cha joto huku wanatanua mabawa yao na wakihema harakaharaka basi joto ni kali/limezidi kiwango. Pale watakapo tawanyika vizuri ndani ya boksi/kibanda cha kulelea huku wanakula na kunywa maji vizuri basi joto ni la wasta na ndilo linalofaa. Kama unatumia njia ya Boksi, basi unatikiwa kulipanua kulingana na ukuaji na mahitaji ya vifaranga vyako.
Vifaranga wako wape chakula cha vifaranga cha kutosha, maji safi na salama, majani mabichi ambayo hufungwa kwa kuning'inizwa kwa kamba,na CHANJO za minyoo nk ili wapate vitamin, madini na protini itakiwayo na kuzuia tabia ya kudonoana ili wakue vizuri.
Hakikisha kuwa chumba chao ni kisafi na hakina unyevunyevu wakati wote. Unyevunyevu husababisha ugonjwa wa baridi na hufanya vifaranga wajikunyate na kutetemeka na wanaweza kufa ghafla!
Inashauriwa kuwa siyo salama kufuga aina nyingine ya ndege kama vile njiwa, bata, bata mzinga nk kwa kuwachanganya na kuku maana kila aina ya ndege wanamagonjwa yao. Hivyo kuwachanganya kutakufanya ushindwe namna ya kuwatibu wanapopatwa na ugonjwa. Pia chawa wa njiwa huleta ugonjwa wa Ndui hasa kuku wanapoangua vifaranga wao. Hapa ugonjwa unaweza kufyeka vifaranga wako wote 60/100 kama utafuata ushauri wangu!
Baada ya wiki 2 hadi 3 baada ya kuwanyang'anya vifaranga kuku wako wataanza tena kutaga mayai. Wakiatamia wote 5 Kama utaimarisha huduma kwao na kwa vifaranga/kuku wale 100 tayari utakuwa una kuku 105 au zaidi. Kuku wale 5 wa mwanzo wakiatamia tena kwa siku 21 hadi 48 (kama utafuata mfumo ule wa mwanzo wa kuaatamishia mara 2) utajipatia vifaranga wengine 100 tena na hivyo kuwa na kuku zaidi ya 200 ndani ya miezi 5/6 tu! Ukiwahudumia vifaranga wale wa mwanzo 100 vizuri kwa miezi 3 na nusu nao wataanza kutaga kama mama zao. kwahiyo, Chukulia walalie majike 5 wa mwanzo na majike 50 waliopatikana baada ya uzao wa kwanza kwa miezi ile 3 ya mwanzo utakuwa na mitetea 55. Wote wakiatamia na watoe vifaranga 10 kila mmoja kwa siku zilezile 21 hadi 46, tayari utakuwa na vifaranga 550! Sasa jumlisha na wale 150 waliobakia kati ya kuku 200 na wote wakakua vizuri utapata kuku na vifaranga zaidi ya 700! Jumlisha na 550 watakaototolewa na mama zao wale 5 wa kwanza na wale 50 wa uzao wa 1 na 2 kwa mara ya 2 si tayari utakuwa na kuku zaidi ya 1,200 ndani ya miezi 6 hadi 8 tu? Hivyo utajikuta unao kuku zaidi ya 1,000!
Kati ya kuku 1,000 ukisema utoe kuku 800 wa kuuza na ukiwauza kwa bei ya Tsh. 4,000 kwa kila kuku 1 tayari utakuwa na Jumla ya Tsh. 3,200,000/= ambazo unaweza kufanya mtaji wa mambo mengine au kuboresha mradi wako zaidi. Unafikiri hapo hujaanza kufikia lengo la kuku 1 akuletee shilingi Milioni 1? Ukiendelea hivi inamaana kuku 1 atakuzalishia zaidi ya hapo.

BANDA LA KUKU.
Unatakiwa kuwa na banda bora la kufugia kuku ambalo litaweza kutunza kuku ili wasiweze kupatwa na madhara mbalimbali kama vile; kuliwa/kujeruhiwa na wanyama wakali, kuchukuliwa na wezi nk. Lakini banda bora pia litawasaidia kuku kuhimili mabadiliko mbalimbali ya hali ya hewa yanayoweza kujitokeza.
Sehemu ambayo inafaa kwa ujenzi wa banda bora ni ile ambayo inaweza kufikika kwa urahisi, iwe na mwanga wa kutosha, isiwe na upepo mkali na isiyoruhusu maji kusimama au kuingia ndani.
Banda ni vema likawa la ukuta/mbao/mabanzi.matete/mianzi imara ili lishikilie paa vizuri lisianguke. Kuta hizi zaweza kujengwa kwa matofali ya saruji/matope/kuchomwa/mabanzi/mbao nk. Katika kuezeka waweza kutumia mabati/vigae/nyasi. Banda ni vema likawa kubwa kulingana na kiasi cha kuku na umri walionao. Kitu cha kuzingatia ni kwamba banda liwe na hewa ya kutosha.
Kuku wanaofugwa ndani ni vema wakatengenezewa uzio mpana (angalau Mita 8x10) ili wapate mahali wanapoweza kuota jua, kupumzikia/kupunga hewa na kufanya mazoezi (wawekee kamba/bembea/ngazi ndani ya banda). Hakikisha kuwa banda ni imara na hawatoki nje ya banda na kwenda mbali ili uweze kuwawekea chakula cha kutosha na maji na hata wale wanaotaga/kuatamia wapate chakula na kurudi haraka.
Banda likiwa kubwa na bora litapunguza magonjwa kwani litakuwa na hewa ya kutosha ambayo itasaidia kupunguza joto na unyevunyevu usio wa lazima bandani mwako. Hii itasaidia uingizaji oksijeni ya kutosha na kupunguza hewa chafu zenye madhara kwa kuku. Pia litasaidia namna ya kufanya usafi kwa urahisi na kupunguza vumbi ambalo linaweza kusababisha kikohozi kwa kuku wako. Ni vema banda lisipungue Mita 3 kwenda juu.
Mambo muhimu ndani ya Banda.
Sakafu nzuri (iliyotengenezwa kwa saruji/udongo ili isituamishe maji. Isiwe na nyufa ili iweze kusafishwa kwa urahisi.
Hakikisha kuwa banda linakuwa na Viota (vitagio) vizuri kwaajili ya kutagia. Viota viwe na urefu wa Sentimita 30 na upana sentimita 30 na kina sentimita 35. Sehemu ya mbele izibwe kwa sentimita 10 tu chini. Sehemu zote hizo zizibwe kwa ubao. Kama kuku wako ni wakubwa unaweza kuongeza upana, urefu na kina kiasi cha kutosha mfano, Upana na Urefu 35cm, kina 55cm nk. Hakikisha kiota/kitagio kinakuwa na giza kiasi maana kuku hupenda kutaga mahala pa giza kidogo/palipojificha. Giza litasaidia kuku asiweze kula mayai au asiweze kudonoana na kuku wengine. Kiota pia kinatakiwa kiwe mahali ambapo ni rahisi kwa kuku kuingia na kutoka, pia iwe ni rahisi kusafisa.
Ndani ya kiota kuwekwe majani makavu/maranda ya mbao laini na kinyunyize dawa ya unga ya kuzuia viroboto/utitiri kabla ya kuweka nyasi.

AIDHA, ni vizuri sana kuwawekea kuku wanaoatamia mayai wakati wa usiku maana ukimuwekea wakati wa mchana anaweza kuyaacha.
Kuku anayetarajiwa kuatamia ni vema akachunguzwa kama anao utitiri/viroboto/chawa kwenye manyoya yake. Wadudu hawa humkosesha raha kuku anayeatamia na wengi huacha mayai na kukimbia/wasitulie kwenye viota vyao. Hali inapelekea kuanguliwa kwa vifaranga wachache. Unaweza kumuona mtaalam wa mifugo kwa ushauri zaidi.
Banda liwe na vichanja maana kuku hupenda kulala juu ya vichanja maana nao ni ndege.
Vyombo safi na vizuri kwaajili ya chakula na maji.
Walazie majani makavu/maranda ya mbao/makapi ya mazao sakafuni kwa banda zima.

UCHAGUZI NA UHIFADHI WA MAYAI.
Mayai huharibika kwa urahisi sana yasipo tayarishwa na kutunzwa vizuri kwa uangalifu. Matayarisho huanzia bandani hadi ndani kwa kufanya yafuatayo;
Hakikisha viota vyote ni safi wakati wote.
Chakula kiwe ni cha kuimarisha gamba la yai na vyakula vingine.
Vyombo vya kukusanyia mayai viewe safi na imara.
Kusanya mayai mara2 hadi 3 kwa siku ili kuepuka mayai kuvunjwa/kuliwa/kuchafuka kwa mayai mengi na kupoa haraka.
Ondoa mayai yaliyo na nyufa na maganda yasiyo imara.
Safisha mayai mara baada ya kukusanya na kabla ya kuweka kwenye chombo cha kuhifadhia saa 12-24. Mayai yanaweza kuoshwa kwa maji ya uvuguvugu (nyuzijoto 35oc) na kusugua taratibu kwa mkono ili kuondoa uchafu (kama upo). Lakini unashauriwa kusugua kwa mkono bila maji ili kusafisha maana maji hupunguza ubora wa yai na maranyingi yai huharibika haraka.
Weka katika vyombo visafi kwa kuelekeza sehemu ya yai iliyo pana iwe juu na sehemu nyembamba iwe chini, beba kwa uangalifu.
Hifadhi mayai katika sehemu ya baridi nyuzijoto10 hadi 16 za sentigredi.
Mayai yapangwe kwa daraja kwa kufuata ukubwa na rangi ili kuvutia wateja na kuongeza bei. Pia unaweza kuweka kwa kufuata muda unapoyaokota kutoka bandani. Weka lebo yenye tarehe ili usichanganye wakati wa kuwaatamishia kuku wako/kuuza.
Kuchagua mayai ya kuatamishia kuku kwaajili ya kuangua vifaranga.
Mayai yanayofaa kwa kuatamiwa na kuanguliwa ni vema yawe na ukubwa wa wastani, yasiwe na ufa/nyufa, yasiwe ya mviringo kama mpira, yasiwe na uchafu wowote juu ya gamba lake, yasiwe yametengwa kwa zaidi ya wiki 1 (siku 7).

NJIA MBALIMBALI ZA UFUGAJI WA KUKU.
Kuna njia kuu mbili za ufugaji wa kuku.
1. Ufugaji Huria
Aina hii ya ufugaji, kuku huachiwa huru wajitafutie chakula na maji wao wenyewe. Utaratibu huu hutumika zaidi kufugia kuku wa kienyeji ambapo mfugaji hupata hasara na pengine hupata faida kidogo maana kuku hukosa uangalizi na hawapewi chakula cha ziada.
Faida.
Haina gharama kubwa za ufugaji.
Kuku hupata mazoezi ya kutosha.
Hasara.
Huharibu mazingira maana hula nafaka, mazao nk.
Ni rahisi kuambukizwa na kusambaza magonjwa.
Ni rahisi kuathiriwa na hali mbaya ya hewa, watu na wanyama wakali kama paka, vicheche, mwewe, kipanga, nyoka nk.
Ni rahisi kutaga mayai porini/vichakani na hivyo mayai/kuku mwenyewe kupotea.
Ukuaji wake ni hafifu/uliodhorota.
Kuna uwezekano wa kuhamia nyumba nyingine/kwa jirani kwa urahisi.

2. Ufugaji wa ndani ya Uzio/Banda.
Hufanyika katika sehemu iliyozungushiwa uzio/ndani ya uzio maalum ambapo kunakuwa kuna utaratibu wa kuku kupewa chakula na maji kwa urahisi. Ndani ya uzio huwekwa banda zuri, bora na imara ambalo huruhusu kuku kuingia na kutoka wanapopumzika/kulala/kutaga mayai. Ufugaji huu hutumika zaidi kwa kuku wa kigeni na kuku chotara na hata wa kienyeji pia.
Faida.
Gharama ya ufugaji wake ni kubwa.
Faida yake ni kubwa hasa ukufuga kibiashara.
Ni rahisi kuelewa kiwango cha utagaji na utotoaji wa kuku wako.
Ni rahisi kufahamu kuku wazuri wa kuatamiashia mayai na kulea kwa faida ya haraka.
Siyo rahisi kuku kuathiriwa na wezi/wanyama/vicheche/mwewe/hali mbaya ya hewa.
Siyo rahisi kuambukizwa magonjwa mbalimbali kutoka nje.
Ni rahisi kutibu na kujua maendeleo ya kuku wako kwa urahisi.
Wanakuwa na usalama wa uhakika.
Faida zake ni nyingi kuliko ufugaji huria.
Hasara
Gharama za mwanzo za ujenzi wa banda, uzio na vifaa vya chakula na maji ni kubwa kiasi. Hivyo zinahitaji mtaji.
Njia hii inahitaji eneo kubwa na huru.
Ni rahisi kuambukizana ugonjwa kama itatokea.
Ufugaji huu unahitaji utaalam na umakini wa kutosha

UCHAGUZI WA KUKU.
Chagua kuku wenye sifa zifuatazo;
Wenye kukua haraka,
Wenye uwezo wa kustahimili magonjwa,
Wanaotaga mayai mengi,
Wawe na uwezo wa kuatamia na kuangua vifaranga wengi na kuwalea (jike/mtetea).
Ni vema sana kutumia majogoo chotara au majogoo wa kienyeji wale wakubwa, warefu, wenye kucha fupi. Chagua wenye maumbile mazuri, uzito wa wastani na wawe wenye rangi za kuvutia kisha uwachanganye na majike/mitetea yenye umbo zuri, uzito mzuri na rangi nzuri ili kupata kuku chotara wanaokua haraka na wenye uzito mzuri kwaajili ya biashara nk. Kama huna kuku wenye sifa hizo basi ni bora sana ukanunua kutoka mahali pengine.
Wakati wa kuatamia ni vema kuku mmoja apewe/awekewe mayai 12 hadi 15 kwenye kiota chake mwenyewe na siyo kuwachanganya kama wakati wa kutaga maayai. Kama wametotoa kuku 2 au zaidi kwa wakati mmoja ni vema aangaliwe kuku mwenye uwezo wa kulea vifaranga ili aachiwe vifaranga vyote (kama utashindwa kuwatengenezea boksi/kibanda cha vifaranga kama nilivyoshauri hapo juu) na kuku wengine watengwe na vifaranga ili waanze kulishwa vizuri na kuchanganywa na majogoo, hapa wataanza kutaga baada ya wiki 2 hivi.
MUHIMU: Ni vema sana kutofautisha makundi ya kuku kulingana na umri wao ili kupunguza kuku kudonoana/kuumizana.

NAMNA BORA YAKULISHA NA KUNYWESHA KUKU.
MAJI.
Maji ni muhimu sana kwa kuku wawapo bandani. Wape maji ya kutosha kila wakati unapoona yanapungua/kuisha ili waendelee kuyeyusha chakula wanachokula Nna kupunguza joto mwilini. Kuku 1 anaweza kunywa hadi robo lita ya maji kwa siku. Kwa hiyo utawawekea kulingana na wingi wao. Pata chombo kizuri ili uwaning'inizie juu kidogo kutoka usawa wa ardhi. Hii itasaidia kupunguza uchafuzi wa maji na magonjwa yanayoenezwa kwa njia ya maji.

ZINGATIA= hakikisha kuwa maji ni safi na salama.
CHAKULA.
Ni vema kutafuta vifaa vizuri kwaajili ya kuwawekea chakula. Tafuta vyombo ambavyo utaweza kuning'iniza/tundika juu kidogo kutoka chini kulingana na umri wa kuku. Hii itasadia sana kupunguza uwezekano wa kutosambaa kwa magonjwa hasa yale yanayoenezwa kupitia viatu tunvyo vaa tunapoingia bandani. Pia itasaidi sana kupunguza chakula kinacho mwagika chini wakati kuku wanapokula.
Kwa mfugaji yeyote wa kuku anapaswa kuelewa kuwa chakula cha kuku ni ghali. Hivyo ni vema kufuata taratibu vizuri katika ulishaji na kutengeneza/kununua vyombo ambavyo kuku hataweza kumwaga chakula. Kumbuka kwamba kama vyombo siyo vizuri basi vitamwaga chakula kingi na hivyo kukuletea hasara.
Ili kuweza kupata mazao mazuri yenye faida, ni vema ununue chakula cha kuku madukani au utengeneze wewe mwenyewe kama nitakavyoeleza hapa chini ili uwape kuku wako chakula chenye viini lishe vyote muhimu kwa kuzingatia umri wa kuku ulionao. Kwa vifaranga, unaweza kuwawekea chakula chini kwenye magazeti/mifuniko ya ndoo/sahani. Baada ya siku 10 unaweza kuwawekea kwenye chombo maalum.

Namna ya kuandaa chakula cha kuku.
Vyakula vya kuku vinapaswa kuwa na aina/viini lishe muhimu kama vile Protini, Wanga, madini na Vitamini.
Vyakula hivyo vimegawanyika kama ifuatavyo;
Vyakula vya kujenga mwili ni; Jamii ya kunde,samaki, dagaa,mashudu ya ufuta/alizeti/pamba,
Vyakula vya kulinda mwili ili usipatwe na maradhi ni; Mafuta ya samaki na majani mabichi kama vile; kabichi, mchicha,majani ya mpapai na nyasi mbichi.
Vyakula vinavyojenga mwili/mifupa ni kama vile; Aina za madini, chokaa, chumvi na mifupa iliyosagwa.
Vyakula vilivyotajwa vinaweza kumkuza vizuri kuku hadi uuzwaji/kuliwa kwake. Surghum Larrymeal huzuia kudonoana, huboresha kiini cha yai na kuongeza mayai. Changanya kg 1 kwa kg 50 za pumba.
Ukosefu wa madini kama fosforasi na kalsiam husababisha matege, vidole kukunjamana, kufyatuka kwa misuli ya magoti, kuwa kilema na kupofuka macho kwa kuku.

Mfugaji wa kuku anaweza kununua vyakula hivi kwenye maduka ya pembejeo za kilimo/mifugo. Na kama huwezi unaweza kujitengenezea wewe mwenyewe.
MAGONJWA YA KUKU.
Kuku huweza kushambuliwa na magonjwa mengi ambayo mara nyingi husababisha hasara kubwa kwa mfugaji. Hasara hizo ni kama vile; gharama za matibabu, upungufu wa mayai, kudumaa kwa kuku, na vifo.

Magonjwa ya kuku yamekuwa ni tishio na hukatisha tamaa sana watu wanaofuga kuku. Magonjwa mengi husababishwa na Bakteria, Virusi, Vimelea, Minyoo, Viroboto, Chawa, Utitiri, Lishe duni au Uchafu. Lakini sauala hili limegundulika kuwa mara nyingi makosa ni ya wafugaji wenyewe kwani maranyingi hupuuzia suala la umuhimu wa kuwaona wataalam wa mifugo (ndege) na baadhi wanapobahatika kuwaona wataalam, basi hupuuzia ushauri wa wataalam hao.

Baadhi ya magonjwa hayo ni kama haya;
1. Kideri au Mdondo

2. Kusinzia

3. Kuhara, Kushusha mabawa chini, kukosa hamu ya kula

4. Ndui au Fowlpox


Tumia njia hizi kukinga magonjwa ya kuku
1. Pilipili kichaa na majivu
2. Katani/Alovera
3. Kitaalam tumia chanjo ya NEWCASTLE.
4. Usafi wa banda &vyombo vote.
5. Usafi wa mazingira na kuchoma moto mizoga yote.
6. Usiruhusu watu kiungia ovyo bandani/usiingize kuku asiyechanjwa.
7. Fuata ushauri wa daktari
Kwa kutumia dawa za asili nilizosema hapo juu;
Pilipili kichaa 50, twanga, changanya na majivu kikombe cha chai 1, weka maji Lita 1 wape kuku.
Katani/alovera. Ipondeponde, iloweke kwenye maji usiku kucha, wape wanywe.
Mkaa. Kama kuku wako wanaharisha,Chukua kiasi cha mkaa, kitwange, changanya kwenye chakula, wape, hawataharisha tena. Mama E.G.White katika kitabu chake cha Uponyaji wa Mungu Uk.64 ameeleza juu ya Tiba ya Mkaa. Jaribu uone mafanikio yake kwa kuku anyeharisha kawaida na siyo kideri.
Kinyesi cha Ng'ombe. Kausha kinyesi cha ng'ombe, kisage na kisha changanya na chakula cha kuku. Hii inasaidia sana kwa kuku wanaonyonyoka manyoya.

MINYOO.
Hawa ni wadudu wanaoleta madhara kwa kuku na wanyama wengine pia. Kuku hupata minyoo kwa kula vyakula vyenye wadudu/vimelea vya wadudu hao.

Dalili. Kuku Hudumaa, manyoya huwa hafifu, hupungua damu na uzito, utagaji wa mayai hupungua, minyoo huweza kuonekana kwenye kinyesi.

Namna ya kuzuia minyoo.
1. Safisha banda mara kwa mara (ukiweza tumia dawa za kuua wadudu)
2. Badilisha matandazo mara kwa mara.
3. Safisha vyombo vya chakula na maji mara 2/3 kwa siku.
4. Tenganisha kuku wakubwa na wadogo.
5. Wape kuku dawa za kuzuia minyoo kila baada ya miezi 3.
6. Muone mtaalam kwa ushauri zaidi.

MAGONJWA YANAYOWEZA KUSABABISHWA NA UPUNGUFU WA CHAKULA/VIINI LISHE.
Iwapo kuku watapewa chakula chenye viini lishe kidogo/kisicho na viini lishe muhimu kama vile; Protini, Wanga, Madini na Vitamini wanaweza kupata madhara yafuatayo;
1. Kudumaa,
2. Kupungua uzito,
3. Kupungukiwa na damu,
4. Mifupa kupinda/kuvimba/kutokuwa imara,
5. Utagaji wa mayai hupungua na uangaji wake pia huwa hafifu,
6. Ganda la yai huwa laini,
7. Manyoya huwa machache na laini,
8. Kujikunja kwa shingo/miguu na vidole,
9. Kuwa na majimengi mazito chini ya ngozi ya kifuani,
10. Kupata magonjwa mara kwa mara,
Hali hii inaweza kusababisha Kuku kufa.

 Namna ya kuzuia.
Kuku wapewe chakula chenye mchanganyiko wa viinilishe vyote muhimu kama vile Vitamini, madini na Chokaa kufuatana na umri/aina na mahitaji yake.
 Wapewe majani mabichi kama mchicha, kabichi na majani ya mapapai.
 Wapewe mchanganyiko wa vitamin na madini kama chokaa na chumvi kwa kiwango maalum maana ikizidi pia yaweza kuathiri kuku.

MUHIMU.
Ili liziua magonjwa ya kuku na kupata faida kubwa kwa kufuga kuku, ni muhimu sana mtu anayehudumia kuku bandani aweze kutambua haraka dalili za magonjwa ya kuku kama nilivyoeleza hapo juu ikiwa ni pamoja na kuzingatia usafi wa banda. Ni lazima ajue tabia ya kuku ya kila siku. Kuku mgonjwa unaweza kumtambua kwa kuangalia yafuatayo;
Tabia ya kuku.
Kinyesi cha kuku (mabadiliko ya kinyesi).
Ulaji wa chakula na unywaji wa maji kama umepungua.
Utagaji wa mayai na uimara wa mayai kama vimepungua.
Kuku kutochangamka.
Vifo ni dalili ya mwisho.
Kama utaona kuna kuku mgonjwa bandani basi mtenge na wenzie kama unavyowafanyia vifaranga. Ili uweze kuwahudumia peke yao. Wengine ambao hawajaonesha dalili wapewe dawa ya kinga haraka iwezekanavyo kupitia ushauri wa mtaalam wa mifugo aliye karibu.

Chanjo na matibabu yoyote yafuate ushauri wa mtaalam/mtengenezaji wa dawa husika bila kupuuzia ili upate mafanikio. Hii itakuwezesha kupunguza/kuponya magonjwa na kupunguza gharama za matibabu na vifo. Hakikisha kuwa chanjo/tiba zinatoka kwa mtaalam anayejua kutunza chanjo/dawa kwenye ubaridi unaotakiwa kulingana na maagizo ya mtengenezaji.

ANGALIZO
Mambo yafuatayo yanaweza kusababisha magonjwa au kupunguza uzalishaji hivyo kuleta hasara zisizo za lazima kwa mfugaji.;
Kufuga kuku wengi kwenye eneo dogo.
Chumba/banda lisilo na hewa na mwanga wa kutosha.
Banda kuwa chafu.
Vyombo vichache/visivyotesheleza kwaajili ya chakula na maji.
Vyombo vichafu vya maji na chakula.
Chakula kisicho na viini lishe vya kutosha/kichache.
Kubadili ladha ya chakula.
Kuchelewa kudhibiti magonjwa ya kuku.
Kuchanja/kutibu kuku bila utaratibu/ushauri wa kitaalam.
Kutishia kuku wakati wa kuingia bandani/kuwashika/kuwasumbuasumbua.
Mabadiliko ya hali ya hewa.
Kufuga kiholela bila kuwachambua.

MWISHO
Ili ufugaji uwe wenye tija kibiashara ufanyike, ni lazma wafugaji tuamke na kuachana na ufugaji wa kuku usio na tija. Nikisema hivi simaanishi watu waache kufuga, hapana, ila wafuge aina /breeds za kuku zenye tija kibiashara. Kuku pekee unaoweza kuwafuga kwa mbinu za kienyeji na bado wakakuletea mfugaji faida nzuri kibiashara, ni kuku aina ya chotara (cross breeds). Hii ni aina ya kuku wenye sifa zote za ukienyeji kwa misingi ya mbinu zao za kuwafuga pamoja na namna walivyo nauwezo wa kuhimili mazingira hasa ya vijijini.

Kuna aina mbalimbali ya kuku hawa ikiwamo Black/ white australorps, kroiller, Rhodes island red, red hamshire, Sussex kama nilivyoanisha hapo awali kwa kiswahili. Hawa ni kuku ambao wanatumika kwa makusudi yote mawili yani  kwa ajili ya mayai na  nyama. Mfano kuku aina ya black/white australorps wao wanauwezo wa kutaga mpaka mayai 250 kwa mwaka, tofauti na wa kienyeji, mayai ya kuku hawa huwa makubwa na yenye kasha jeupe na kiini cha njano kama utawafuga kwenye mazingira na mbinu asilia (za kienyeji).

Ukilinganisha uwezo wa utagaji wa kuku hawa utagundua utagaji wao ni Zaidi ya asilimia 500% ukilinganisha na ule wa kienyeji kabisa. Idadi hii ya mayai toka kwa kuku mmoja kwa mwaka, anaweza kumwezesha mfugaji kuzalisha mayai kwa wingi na kushusha Zaidi bei ya mazao yake (mayai) kuwa chini kuweza kuliteka soko kwa urahisi Zaidi. Kumbuka, bei ya juu ya mayai ya kienyeji ni kwaajili ya kulipia gharama kubwa za utunzaji wa kuku huyu ilihali utagaji wake ni hafifu.

Pia, kuku hawa wana nyama nyingi Zaidi kuliko hawa wa kienyeji kwa majogoo hufikia mpaka uzito wa kilo 3-3.5. huku matetea hufikia kilo 2-2.5 na huwa na nyama nzuri, iliyokomaa vyema na yenye ladha. kwa uzito huu kwa majogoo, kuku hawa uuzwa kwa bei ya 20,000 - 25,000 wakiwa hai. bei ambayoni kwa mujibu wa bei ya soko kwa makadirio ya shilingi 8,000 kwa kilo kwa nyama nyeupe.
Chagua njia bora na rahisi inayokufaa kulingana na eneo ulilopo na mahitaji yako pia. Angalia njia itakayokupa faida kwa gharama ndogo.
Chagua kuku wenye uwezo wa kukua haraka, wanaostahimili magonjwa, wanaotaga mayai mengi, wanaoweza kuangua vifaranga wengi na kuwalea.
Chagua jogoo aliye na uzito mzuri na mwenye kucha fupi.
Uwiano wa jogoo kwa majike iwe ni jogoo 1 kwa majike/mitetea 10.
Kuku anayetazamiwa kuatamia mayai anatakiwa asiwe na chawa/viroboto/utitiri.
Kuku ambaye hakidhi sifa za kuwa kuku bora anayefaa kuwa kwenye kundi inafaa aondolewe ili asilishwe kwa hasara awapo bandani.
Waafrika tulio wengi hatuna utamaduni wa kutunza kumbukumbu. Ni vizuri basi uanze kutunza kumbukumbu za mwenendo wa kazi zako za ufugaji wa kuku. Hii itakurahishia sana kujua faida, hasara na hata kujua namna bora ya kuboresha ufugaji wako. Kwa mfano;
Kumbukumbu za uzalishaji mayai zitakuwezesha kujua kiasi cha mayai yanayotagwa kwa siku. Idadi ikiwa chini ya 60% utagaji huo siyo mzuri hivyo utatafuta sababu ya tatizo nk. Utagaji unatakiwa uwe 70% hadi 95%.
Kumbukumbu ya vifo itakusaidia kujua hatari itakayokujia. Mfano vifo vikizidi 1% inaashiria tatizo la ugonjwa. Hivyo uchunguzi ni lazima ufanyike ili kutatua tatizo.
Kumbukumbu za mapato na matumizi pia zitakusaidia kujua faida na hasara nk. Hapa utajua ni ghara kiasi gani ulitumia kufuga na faida kiasi gani umepata baada ya mauzo ya mayai/kuku husika.

Comments

Popular Posts