Kilimo na ufugaji sehemu ya kwanza



Miaka mitatu iliyopita nilipata hamasa ya kujiingiza katika kilimo baada ya kugundua faida zilizopo katika kilimo, niliandika michanganuo mingi ya mazao mbali mbali nikajaribu kuzungumza na watu wangu wa karibu lakini kila mahali nilikatishwa tamaa kutokana na watu kukosa uelewa wa utajiri uliopo katika kilimo. pamoja na kukatishwa tamaa pia sikua na mtaji wa kuanzia bali wazo tu nililoweka katika karatasi. kama usemavyo ule msemo unaosema kila jambo au tuseme mradi ulianzia kwenye wazo, hivyo mwaka uliopita nilipata mtaji na nikajiingiza katika sekta  hii ya kilimo cha kitunguu na ufugaji wa kuku wa kienyeji. Na nikapata nafasi ya kujifunza mambo mengi ambayo ninapenda nishirikiane nanyi katika makala hii na makala zifuatazo ikiwa ni mtiririko wa biashara ya kilimo na ufugaji. waswahili wanasema, kizuri kula na ndugu yako.

Katika uwekezaji kuna misemo miwili ya kiingereza ambayo ni capital gains (ongezeko la mtaji) na cashflow (mtiririko wa fedha). Kila mtu anayetaka kuwekeza fedha yake mahali Fulani ili apate faida hupitia katika mojawapo ya njia hizi mbili, sasa hili ni somo pana kwa ajili ya siku nyingine lakini kwa ufupi capital gains ni pale unapoweka fedha yako mahali na kutegemea kwamba itapanda thamani pale utakapofikia mwisho wa uwekezaji, mfano umenunua nyumba ml30 halafu baada ya muda eneo lile likapanda thamani na kuwa mjini ukaiuza nyumba hiyo kwa ml80, ml50 ni capital gains, vivyo hivyo katika kilimo, na baadhi ya mifumo ya ufugaji. Pia cashflow ni pale unapowekeza fedha yako mahali na ikakupatia mtiririko wa fedha wa kila siku, wiki, au mwezi. Mfano mzuri ni pale unapowekeza katika biashara ya dala dala, duka, taksi, nk.

Leo tutazungumzia capital gains katika sekta ya kilimo na katika sehemu ya pili tutazungumzia katika upande wa ufugaji
Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na mwamko mkubwa katika sekta ya kilimo na ufugaji. Sekta ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikifanywa na watanzania walioaminika kuwa masikini. Lakini ndugu msomaji ninapenda kukupatia taarifa kwamba sekta hii kwa miaka ya hivi karibuni imeinua watanzania wengi waliokuwa na nia, ujuzi, nyenzo, na mpango madhubuti waliojihusisha katika sekta hizi mbili.

Ufugaji wa kuku wa kienyeji kwa muda mrefu imekua ikifahamika kuwa kazi ya wakina mama, lakini siku  za hivi karibuni wakina baba na baadhi ya vijana wamefunguka akili na kuona umuhimu wa kujihusisha katika sekta hii kwani imekuwa na faida nyingi. Pamoja na hayo kuna aina nyingi za ufugaji kutegemea na kile mhusika anachopendelea kujihusisha kwacho kwani kuna

1. Ufugaji wa kuku, kware na bata mzinga
2. Ufugaji wa samaki
3. Ufugaji wa ng’ombe, mbuzi, na kondoo
4. Pamoja na ufugaji wa mbwa kwa ajili ya biashara


Zote hizi ni fursa katika sekta ya ufugaji na katika jamii zetu kuna mifano hai ya watu waliojihusisha katika ufugaji wa wanyama hao na kujipatia mtaji na namna ya kuendesha maisha. Katika makala ijayo tutazungumzia kwa undani sekta hii na kupitia baadhi ya michanganuo ya uwekezaji na faida inayopatikana.

Kilimo ni biashara kama ilivyo biashara zingine pale inapofanywa kwa ufasaha na kwa mpangilio maalum, na kwa namna hiyo kina uwezo wa kurudisha fedha uliyowekeza pamoja na faida.
Katika sekta ya Kilimo kuna aina tatu za kilimo;
1. Kilimo cha umwagiliaji
2. Kilimo cha msimu (wa mvua)
3. Kilimo cha mazao ya muda mrefu
4. Kilimo cha ndani nyumba ya kuhifadhia mimea (Greenhouse)

Sekta ya kilimo ni uwanja mkubwa unaotoa kipato kikubwa kwa watanzania wachache kwa sababu wachache hao wamekuwa tayari kuenda na wakati na kuacha kilimo cha kamari yaani kilimo cha kutegemea mvua. Ni kweli mvua ni za muhimu katika kilimo cha mazao ya muda mrefu mfano mazao ya matunda kama machungwa, maembe, tufaa nk. Lakini inapokuja katika suala la kupata fedha uliyowekeza haraka na kwa faida nzuri kilimo bora ni kilimo cha umwagiliaji. Pamoja na yote ni vyema kutambua kuwa kilimo pia kinaweza kikawa shimo la kuzikia fedha zako endapo hakitafanywa kwa umakini na mpangilio mzuri.
Aina za mazao yenye faida
Kama nilivyosema hapo awali kilimo cha umwagiliaji ndio kilimo chenye faida lakini pia watanzania wengi wamejihusisha katika kilimo cha mazao ya muda mrefu na kupata faida kubwa. na haya ni baadhi ya mazao yenye faida;
1. Kilimo cha mboga mboga mfano vitunguu, nyanya, hoho, bamia nk.
2. Kilimo cha nafaka kama vile mahindi, ufuta, alizeti, ngano, nk.
3. Kilimo cha matunda mfano tufaa (apples), maembe, mananasi, machungwa nk.
4. Kilimo cha mizizi kama vile viazi, mihogo na magimbi.

Katika makala hii tutajikita katika kilimo cha vitunguu. Kilimo ambacho kinaweza kikafanyika ndani ya greenhouse,

 kinaweza kikafanyika kutegemea mvua na pia kwa kumwagilia. Njia ya umwagiliaji (Irrigation) hadi sasa imethibitika  kuwa na uhakika wa mafanikio.

Vitunguu ni moja ya zao la bustani linalopendwa na kutumiwa kwa wingi sana si hapa nchini tu bali duniani kote kwa ujumla. Linachukua nafasi ya pili baada ya nyanya. Kitunguu kinatumika katika kachumbari, kama kiungo kwenye kitoweo kama vile Samaki, nyama, mboga za mahani n.k. Majani ya vitunguu hutumika kama mboga. Vitnguu pia hutumika kuandalia supu.



Vitunguu hustawi maeneo yasiyo na mvua nyingi sana, yenye baridi kiasi wakati wa kiangazi na maeneo yasiyo na joto kali pamoja na ufukuto wa ukungu wakati wa kukomaa kwa vitunguu.

Vitunguu hustawi vizuri kwenye udongo wenye rutuba ya kutosha, unaoruhusu mizizi kupenya na unaohifadhi unyevu kama vile udongo wa nusu mfinyanzi nusu tifutifu.

Mchanganuo wa kilimo cha vitunguu kwa ufupi katika mkoa wa manyara ni kama ifuatavyo;
1. Kukodi shamba kwa heka moja ni kati ya sh 80,000 hadi sh 150,000 kulingana na eneo husika
2. Kulima kwa trekta ni sh 50,000 kwa heka, na hii hutegemea aina ya shamba ulilopata kwani unaweza ukalima majembe mawili na haro au jembe moja na haro. Hivyo kuwa angalau 100,000
3. Mashine ya kumwagilia na pipe zake 650,000 (ni vyema ukatafuta mtu aliye na mashine na kuingia nae mkataba, au unaweza kukodisha.)
4. Mbegu kopo sita, kila moja 60,000
5. Kutengeneza majaruba 150,000
6. kupanda 100,000
7. mafuta kwa ajili ya kumwagilia lita 5 (2500*5=12,500) angalau kila wiki mara moja kwa siku tisini au wiki 12: 12,500*12= 150,000
8. madawa kwa ajili magonjwa na wadudu kwa msimu mzima 200,000
9. palizi ya kwanza na ya pili 200,000 (hii hutegemea na shamba sehemu zingine palizi huwa hadi mara tatu)
10. mbolea ya urea 45,000 kwa kilo50 na 45,000 kwa mbolea ya CAN
11. vifaa vya kazi 50,000
12. vifaa vya kambi 450,000 endapo kutakuwa na kambi kwa ajili ya wafanyakazi na sehemu ya kutunzia vifaa
13. uvunaji 150,000
14. usafiri 200,000 (hii ni kwa ajili ya mizunguko ya kutafuta dawa, kununua mbolea, pamoja na mizunguko mingine, kwa hiyo itategemea mtu na mtu)
15. dharura 200,000

16. chakula kwa ajili ya wafanyakazi itategemea na ni watu wangapi utakuwa nao shambani, kwani unaweza ukaajiri watu kwa makubaliano ya kulipana mwisho wa msimu, au unaweza ukawa na msimamizi mmoja na vibarua wakatafutwa pale watakapohitajika.
Jumla ya mchanganuo huu rahisi wa kilimo cha kitunguu kwa heka moja ni 2,700,000. Ambapo inakadiriwa heka moja ina uwezo wa kutoa gunia 80 hadi 100 kulingana na ufanisi uliowekwa katika mradi mzima, ubora wa mbegu, pamoja na ardhi na magonjwa. Hivi huchangia sana katika kuongeza au kupunguza mavuno.

Namna ya kulima kitunguu ni kama ifuatavyo

UPANDAJI WA MBEGU ZA VITUNGUU KWENYE KITALU.


Hapa kwetu Tanzania upandaji huanza mwezi March hadi Mei kutegemea na msimu wa kilimo ulivyo. Hivyo kilimo hiki huanza mara baada ya mvua kubwa za masika kumalizika. Kipindi cha kiangazi na baridi huruhusu ukuaji mzuri wa vitunguu.

Mbegu za vitunguu huoteshwa mapema katika kitalu. Mbegu zinaweza kutawanywa au kupandwa kwa mistari katika tuta la kitalu.Tengeneza matuta yenye upana wa mita 1 na urefu wowote kutegemea na mahitaji yako.Weka mbolea ya samadi ndoo moja hadi mbili kwa mraba wa mita moja.
Lima tuta kiasi cha sentimita 10-25.
Sia mbegu katika mistari yenye nafasi ya sentimita 15 kutoka mstari hadi mstari Katika upandaji wa mstari mbegu hupandwa katika nafasi ya sm 10 hadi 15 kati ya mstari na mstari. Gramu 5 (kijiko cha chai) zinatosha kusia eneo la mraba mita moja.
Tandaza nyasi na mwagilia.


Baada ya kupanda mbegu hufunikwa na udongo mwepesi na baadaye matandazo juu ya tuta. Mara baada ya mbegu kuota matandazo yaondolewe na badala yake kichanja cha nyasi kijengwe ili kuiwekea kivuli miche michanga. Mbegu za vitunguu huota baada ya siku 7 hadi 10.

KUMBUKA KAMA UNATAKA KUWA MKULIMA NA ULIME ZAO LA VITUNGUU: Kilo 1.5 za mbegu zinatosha hekari moja ya shamba.

KUPANDIKIZA MICHE BUSTANINI(kutoka kwenye kitalu kwenda shambani)

Upandikizaji wa miche ya vitunguu hufanyika baada ya miche kukua na kufikia unene wa Penseli. Mara nyingi miche hii hukaa kwenye kitalu kwa siku 40 baada ya kupandwa.

Usichelewe kuhamishia miche yako bustanini maana ukipandikiza miche mikubwa itaanza kutoa maua badala ya kitunguu (bulbs). Hivyo mara nyingi miche ya namna hii hubaki na suke la maua.

Wakati wa kupandikiza usikate wala kupunguza majani. Miche ipandikizwe sm 30 kati ya mstari na mstari na sm 10 kati ya mche na mche.

Upandaji katika bustani hufanyika kwenye mistari katika matuta au kwenye vijaruba. Vijaruba hutumika katika maeneo tambarare na yenye ukame ili kuhifadhi unyevu baada ya kumwagilia. Sehemu zenye udongo mzito na wenye maji mengi tumia matuta yenye mwinuko wa sm 10 hadi sm 15 kutoka usawa wa ardhi.
KUMBUKA: Pandikiza miche wakati wa asubuhi au jioni na mwagilia maji ya kutosha lakini hakikisha maji hayatuami.

UWEKAJI WA MBOLEA

Weka mbolea ya kukuzia katika wiki ya nne hadi sita baada ya kupandikiza. Weka mbolea kwenye mstari na hakikisha isigusane na mimea. Hakikisha udongo una unyevu wa kutosha wakati wa kuweka mbolea. Tumia UREA au SA.

UMWAGILIAJI



Zao la vitunguu linahitaji maji katika kipindi chote cha ukuaji wa mmea na hasa wakati wa utungaji wa tunguu (bulb).

Katika kipindi kisicho na mvua, miezi ya mei hadi Agost, umwagiliaji ufanyike mara moja kwa wiki Pia katika umwagiaji hutegemea sana na aina ya udongo katika shamba lako kwa sisi wataalamu kama tunajua aina ya udongo uliopo shambani kwako tutaweza kukuambia inatakiwa umwagilie kwa muda gani na unatakiwa umwagilie tena baada ya siku ngapi.


Ili kuharakisha kukomaa kwa vitunguu, unashauriwa kupunguza kiasi cha maji kadri vitunguu vinapoendelea kukua. Pia ni vema uache kumwagilia maji wiki nne hadi sita kabla ya kuvuna. Kwani muda kamili wa kukomaa vitunguu na kuvuna ni siku 90 hadi 120 kutegemeana na aina ya mbegu.



KUDHIBITI MAGUGU(PALIZI) NA KUPANDISHIA UDONGO.

Kitunguu ni zao lisiloweza kuvumilia magugu, magugu husababisha kupungua kwa ukubwa wa kitunguu, hueneza magonjwa na husababisha kudumaa kwa kitunguu.

Katika bustani ya vitunguu, magugu yanaweza kung'olewa kwa kutumia jembe dogo la mkono, kung'olea kwa mkono au kwa kutumia madawa ya kuulia magugu (herbicides).

KUMBUKA: Unapotifulia, epuka kutifua kwa kina kirefu maana utaharibu udongo na vitunguu vyenyewe kwa kuwa mizizi ya vitunguu ipo juu juu sana.


Kupandishia udongo kwenye mashina ya vitunguu ni hatua muhimu ili vitunguu visiunguzwe na jua. Hakikisha kwamba mashina ya vitunguu vyako yako ndani walau sm 5. Pia kuna aina nyingine ya vitunguu ambavyo hutoa au hupandisha tunguu lake juu ya udongo vinapokua. Hivyo kupandishia udongo ili kufunika tunguu ni muhimu sana.
Hakikisha shamba linakuwa safi. Wakati wa kupalili, mkulima asichimbue sana udongo ili kuepuka mikwaruzano kwenye shina la vitunguu. Inulia udongo kwenye mashina kama mkulima amepanda sesa.

MAGONJWA NA WADUDU WAHARIBIFU.

Wadudu waharibifu.

Kuna aina mbili za wadudu wanaoharibu hili zao;

1. Viroboto wa vitunguu



Hawa ni wadudu waharibifu namba moja wa zao vitunguu hapa nchini kwetu Tanzania. Husababisha upotevu mkubwa wakati wa mavuno. Wadudu hawa huonekana hasa kipindi cha joto.

Dalili.

Majani yaliyoshambuliwa na wadudu hawa huwa na mabaka meupe yenye kung'aa. Katika hali iliyokithiri majani yote huwa na tabaka jeupe au kijivu na baadaye hunyauka kabisa.

Kuzuia.

Mdudu huyu huzuiwa kwa kupiga dawa ya kuulia wadudu (insecticide) kama vile Marathion, Thiodan-35, Parathion

Ili kupunguza uvamizi mkubwa panga kupanda vitunguu mapema ili kipindi cha joto kinapofika kikute vitunguu vyako vimekomaa.

Epuka kupanda vitunguu katika shamba lililokuwa limepandwa jamii ya vitunguu hapo kabla kama vile liksi, vitunguu swaumu, n.k.
3. Bungua weupe (White grub)


Huyu ni aina ya funza mkubwa,. Hutaga mayai yake kwenye uozo wa majani na samadi na hivyo mashamba ya vitunguu yaliyoko karibu hata kwenye maeneo au mashamba karibu huwa kwenye hatari zaidi. Mdudu huyu huathiri kitunguu kwa kukata miche na minyoo wa vitunguu.
Hushambulia mizizi na kusababisha kukauka kwa mimea.
 Kutifulia shamba na kuwaweka wazi wadudu hawa kunapunguza idadi yao.
Pia Hawa huzuiwa kwa kuzingatia mzunguko wa mazao


MAGONJWA.

1. Ukungu mweupe.



Ugonjwa huu huonekana wakati wa baridi ulioambatana na unyevu mwingi angani.

Dalili.

* Utaona unga unga wa rangi ya zambarau katika majani.
* Majani hugeuka rangi na kuwa ya njano na kisha hunyauka.
* Ugonjwa huu hupenya hadi chini kwenye tunguu na husababisha kuoza.

KUZUIA

Fanya kilimo cha mzunguko ukihakikisha unapanda mazao mengine yasiyo jamii ya vitunguu. Panda vitunguu tena baada ya miaka mitatu kama athari ilikuwa kubwa.

Tumia dawa za ukungu (fungicides) kunyunyizia katika shamba. Hii ifanyike kabla ya dalili kuonekana. Tumia dawa kama Zineb ya unga, Maneb, Dithane M45, n.k.

Wakati unapoona dalili za hali ya hewa yenye baridi ikiambatana unyevunyevu angani. Katika kipindi hiki piga dawa kila baada ya siku sita ili kuzuia ugonjwa kuingia.
Ugonjwa ukishaingia kwenye mmea hauzuiliki kwani hakuna dawa ya kuponesha.

2. Ukungu wa kahawia.


Ugonjwa huu huleta madhara makubwa wakati vitunguu vikiwa bustanini na hata wakati vitunguu viko ghalani.

Dalili.

Vikovu mbonyeo hujitokeza kwenye majani na baadaye huwa na rangi ya zambarau. Vikovu hivi hukua na kutengeneza vidonda ambavyo hukua na kufanya mzunguko katika jani zima au katika shina la kitunguu. Baada ya wiki kama tatu tangu kuingia kwa ugonjwa huu, majani yote huanguka na kidmsha kukauka.

Ugonjwa huu hushambulia kitunguu hata baada ya kuvuna kupitia sehemu ya shingo ya kitunguu au sehemu yoyote yenye kovu, kidonda au mkwaruzo.

 NAMNA YA KUZUIA

*Katika bustani, unapoona kitunguu kina dalili ya ugonjwa huu, ng'oa na choma.
* Kwa kinga ya bustani, piga dawa za Dithane M45 na dawa zingine za ukungu. Dawa hizi hupunguza uwezekano wa kuenea kwa ugonjwa huu.
* Tumia kilimo cha mzunguko wa mazao katika eneo la bustani yako. Usipande vitunguu katika mzunguko wa jamii ya vitunguu.
* Wakati wa kuvuna epuka kukata vitunguu na kusababisha vidonda na makovu.
* Ukishavuna anika kwa siku mbili kabla ya kuhifadhi kwenye magunia.

3. Ugonjwa wa kuoza mizizi

Huu ni ugonjwa unaotoka udongoni na huenezwa na vimelea vya Ukungu (fungi).

Dalili

Mizizi kugeuka rangi na kuwa njano na kisha zambarau. Baada ya muda ugonjwa huenea na mizizi hufa kwa kunyauka.

KUZUIA

Panda vitunguu kwa mzunguko wa mazao. Epuka kurudia kupanda vitunguu kwa mfululizo.

Panda aina za mbegu zinazostahilimili magonjwa kama;
Excel, L36, Granex, White Granex, Red creole.

4.  Ugonjwa wa doa la pinki (Purple blotch)



Uanza kama doa dogo linalozama ndani ya jani na kisha
linaongezeka ukubwa na kufanya rangi ya pinki. Kiini cha ugonjwa
huu huanzia kwenye mbegu na pia hubaki kwenye maozo ya majani
ya vitunguu. Aina ya Red Creole inaonyesha kutoshambuliwa sana
na ugonjwa huu.
Ugonjwa wa doa la pinki Kuoza kwa kitunguu
Mbinu za kudhibiti ugonjwa huu ni kuendesha mzunguko (crop
rotation) wa muda mrefu wa mazao pamoja na kuzuia kutuama kwa
maji shambani. Kupunguza msongamano wa mazao shambani na
matumizi ya mbolea zenye calcium, phosphate and potassium
hupunguza kuenea kwa ugonjwa huu. Kwa upande mwingine,
matumizi ya mbolea ya nitrojeni kwa wingi au kwa kiasi pungufu
uongeza mlipuko wa magonjwa. Viatilifu kama vile Mancozeb
hutumika kuzuia mashmbulizi ya ugonjwa huu.

UVUNAJI WA VITUNGUU



Kwa ujumla uvunaji wa vitunguu huanza siku 90 hadi 150 tangu kwa miche kupandwa yaani miezi mitatu hadi mitano tangu kupandikizwa bustanini kutegemeana na mbegu iliyopandwa.

Utagundua kuwa vitunguu vyako viko tayari kuvunwa unapoona karibu 50% au zaidi ya mazao shambani yanaanguka au majani kukauka.

Ili kurahisisha ukaushaji wa vitunguu, pangilia muda wako ili uvunaji ukutane na kipindi cha joto na kiangazi.
Uvunaji ufanywe kwa kung'oa baada ya kumwagilia maji bustani siku moja kabla ya kuvuna.
Baada ya kuvuna, kata majani sm 2 juu na kata mizizi sm 2 chini. Usikate chini sana ya shingo maana husababisha jeraha na kupelekea kitunguu kuoza.
KUMBUKA:Ucheleweshaji wa uvunaji unasababisha vitunguu kuoza na kuharibikia shambani. pia Tumia jembe la mkono na hakikisha vitunguu havikwaruzwi wakati wa kuvuna. Unaweza kuvuna tani 30-40 kwa hekta.
Changamoto
Baada ya kukupitisha katika taarifa hizo hapo awali, ninapenda kukutahadharisha kwamba kilimo hakipaswi kufanywa bila mpangilio uzoefuna ujuzi mahsusi katika zao husika. Kwani jambo dogo linaweza likakusababishia hasara kubwa kwa sababu tu ya kukosa uzoefu au kukosa ujuzi wa jambo hilo. Mfano kutokana na mkulima kukosa uzoefu mazao yake hushambuliwa na wadudu na magonjwa ambayo hayafahamu na yakapunguza mavuno au mkulima akakosa mavuno kabisa.
Lakini pia kumekua na changamoto ya madalali wa mazao kuwalalia wakulima kwa muda mrefu. Bei ya kitunguu ni 40,000 hadi 180,000 kwa gunia kulingana na uhitaji wa kitunguu sokoni. Pamoja na hayo matajiri wachache wenye hekari nyingi za kitunguu hutajirika kwa kupeleka nje ya nnchi hasa Kenya, Uganda, Kongo, Sudan na Somalia.

Mifano ya waliofanikiwa
Mifano mizuri ya watanzania waliofanikiwa kutokana na kilimo ni pamoja na
1. Masanja Mkandamizaji ambaye ni mkulima wa  mpunga amepata mafanikio mengi ambayo yametokana na kilimo pamoja na shughuli zake zingine.


2. Eric Shigongo ambaye ni mkulima wa mananasi maeneo ya pwani amefanikiwa kujenga hoteli kupitia kilimo na biashara zake zingine.

Nilianza kwa kukuambia aina mbili za uwekezaji ambazo ni uwekezaji kwa ajili ya kukuza mtaji na uwekezaji kwa ajili ya mtiririko wa fedha. Pamoja na kilimo kuwa ni uwekezaji wa kukuza mtaji/fedha pia kilimo kinaweza kikawa ni uwekezaji wa kukupatia mtiririko wa fedha kwani biashara ya ulimaji wa mashamba kwa trekta una fungua bomba la mtiririko wa fedha. Unaweza ukanunua trekta na kulitumia kulimia mashamba ya watu kwa 50,000 heka na ikakupatia mtiririko wa fedha kila siku. Lakini pia kwa wale wasiokuwa na mtaji wa kununua trekta unaweza ukakodisha trekta kwa mtu na ukalitumia kulimia mashamba ya watu na kupata faida katika tofauti ya fedha uliyokodisha trekta kwa msimu na fedha uliyokodisha trekta kwa mmiliki wake. Pande zote mbili kilimo ni biashara yenye faida pale inapofanywa kwa weledi, umakini na mpangilio maalum wa kibiashara.
pamoja na hayo nitakuletea pia fursa zingine zilizopo katika sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na kilimo cha matufaa (apples) kilimo cha miti na mazao ya muda mrefu.
Tukutane katika sehemu ya pili


Comments

Popular Posts