Tundu Lissu; Unaweza Ukajifunza nini kwake?



Mambo ya kujifunza kutoka kwa Mwanasheria Msomi.
Tundu Lissu kama tunavyofahamu ni mtanzania aliyezaliwa mwaka 1968 tarehe 20, Januari. Na ni mbunge wa Singida mjini ambaye alitoka mjini alikokulia na kwenda mbali na akakutana na watu mbalimbali wa tofauti, akapata (exposure) nafasi ya kuona mengi na hiyo ikamjenga kuwa Tundu Lissu huyu tunayemfahamu.
Hakuzaliwa mjini bali alizaliwa katika kijiji kidogo cha Mahambe huko Singida, kwa wazazi waliokuwa na hali duni. Japo baba yake alikuwa mwenyekiti wa kijiji lakini bado wakati ule wa ujamaa hali bado ilikuwa ni ya umaskini kwa watanzania wengi. Maisha ya Mwanasheria huyu aliyeshinda Uraisi wa Chama cha Wanasheria kutoka kuwa mwanafunzi aliyefundishwa na waalimu ambao hawakusomea ualimu, ni jambo la kuangalia.
Shule ya Msingi
Maisha ya Shule ya Msingi ya Tundu Lissu ni ya kushangaza, kwani hapakuwa na shule katika kijiji chao na walisoma darasa la kwanza kwenye nyumba iliyotolewa na mwanakijiji, na wao ndio walikuwa wanafunzi wa katika kijiji chao. Darasa la mwaka 1976, akiwa na miaka 8. Baba yake alikua amesoma hadi darasa la sita kwa wakati huo, na mama yake hakuwa amesoma hata darasa moja. Hivyo waliona umuhimu wa elimu na Tundu na wenzake wakasoma hadi darasa la saba kutokana na wahisani ambao walikuwa ni wanakijiji, na padre wa eneo la kwao.
Ø  Unaweza ukaona Umuhimu wa elimu katika kufikia lengo ulilo nalo, kwani elimu hukupatia dira ya kile unachopaswa kufanya kwa wakati husika. Lakini pia bila kuzingatia aina moja tu ya elimu, kuna elimu ya dini,  elimu ya darasani, na elimu ya maisha.
Ø  Tabia ya Uanaharakati au uasi kwa maneno makavu haikuanza alipokuwa mwanasheria bali ilianza tangu akiwa mtoto kwani alikuwa na tabia ya kumhoji baba yake juu ya uhalali wa wao kuhamishwa kutoka kwenye kijiji chao na kuelekezwa kwenye vijiji vya ujamaa.

Pamoja na hayo, elimu yake ya shule ya msingi kwa sehemu kubwa aliipata kutoka kwa waalimu ambao hawakuwa wamesomea ualimu kwa sababu ya uhaba wa waalimu kijijini kwao.

Shule ya Sekondari
Tundu Lissu alikuwa na uwezo wa kiakili tangu akiwa kijana mdogo, kwani kutoka kwenye kijiji cha ndani ndani huko Singida aliweza kupata nafasi ya kusomea Ilboru Sekondari Jijini Arusha. Na akaanza kujifunza vitu vingi na kukutana na watu wengi ambao waliweza kuweka mguso Fulani kwenye maisha yake.
Ni wazi kwamba Tundu Lissu ni “Mwanaharakati” lakini uanaharakati huo haukuibuka ghafla tu. Alianza kuwa mwanaharakati tangu akiwa kijana mdogo na safari yake inaanza pale alipoanzisha Kampeni ya kupinga baadhi ya wanafunzi kutoruhusiwa kwenda Korogwe Girls Kucheza na wanafunzi wa shule hiyo.
Ø  Nyota njema Huonekana Asubuhi; kipaji kinapoonekana tangu utotoni na kuendelezwa huwa na nguvu sana katika utu uzima. Lakini pia wakati wowote unafaa kuanza kuwa kile unachoamini.
Ø  Hakuna Utii Penye Shuruti; ilimbidi Tundu kuwa na kadi ya mwanachama wa CCM ili kupokelewa shule ya Sekondari, na kama kawaida yake hakuweza kujizuia kuonyesha hali yake ya kutokuridhika na sheria hiyo na hiyo kuwa moja ya chachu iliyomfanya kuwa Tundu Lissu wa leo.
 Chuo kikuu
Kabla Lissu hajapata nafasi ya kuenda chuo kwanza ilimbidi kwenda JKT kama ilivyo desturi. Na kule pia aliendeleza tabia yake ya “uasi” hadi kufikia kiwango cha kujibizana na Kanali wa Jeshi ambaye alikuwa Omar Mahita kwa wakati huo na hii ikamfanya kuanza kujenga maadui katika mfumo.
Pigania kile unachoamini. Pale Tundu Lissu alipoona haki ikipindishwa kwa mtazamo wake. Alisimama kidete ili kuhakikisha haki hiyo inapatikana. Akiwa kijana mdogo tu wa miaka 27 aliweza kwenda marekani kutokana na juhudi zake za kupigania haki zilivyokuwa na msaada mkubwa kwa wananchi, mfano mmoja ni mradi wa ufugaji kamba delta ya Rufiji. Mradi wa Mzungu mmoja wa Ireland aliyeitwa Reginald Nolan. Alipewa na Serikali ya Rais wa Awamu ya Tatu Mh.Mkapa hekta 20,000 ili atengeneze mabwawa ya kufuga kamba kwenye delta ya Rufiji katika maeneo ambayo yana vijiji karibu vinane, ambapo watu walikuwa wanalima na kuishi. Tundu Lissu na Kampuni aliyokuwa akifanyia kazi, kupitia Chama Cha Wanasheria wa Mazingira – LEAT, waliusimamia kidete mradi huo hadi ukafungwa. Aliratibu kampeni za kimataifa kwa kila njia, ikiwamo mitandao ya kimataifa ya wanaharakati kuupinga huo mradi.
Hatimaye, Benki ya Vitega Uchumi ya Ulaya (European Investment Bank) iliyokuwa itoe mkopo ambao ungedhaminiwa na Serikali ya Tanzania wakaahirisha kutoa mkopo huo na mradi ukaisha.


Ø  Kuwa na maadui hakuepukiki lakini usitengeneze maadui kwa makusudi kwani inaweza ikawa mwisho wa safari yako ya kufikia malengo yako. Tunaweza tukakumbuka mifano ya wanaharakati wengi waliouawa kwa sababu ya kujijengea uadui na watu bila ya sababu za msingi mfano mzuri ni Iddi Amin ambaye hulka yake ilimfanya kuwa na maadui wengi ambao waliikatisha safari yake ya uongozi, mfano mwingine mzuri ni Chacha Wangwe aliyekuwa Mbunge wa Jamhuri.

Changamoto alizopitia
Ø  Tundu Lissu amewahi kufungwa mara nne na mara kadhaa kuwekwa kizuizini kwa sababu ya hulka yake ya uchochezi wa mambo hali inayomfanya kuwa kwenye macho ya adui zake kwa muda mrefu.
Ø  Tundu Lissu amepitia matukio kadhaa ya kudhalilishwa akiwa uraiani ikiwemo kukamatwa na polisi pamoja na kudhalilishwa bungeni na kufukuzwa bungeni mbele ya wananchi. Lakini hiyo haikumzuia kupigania kile anachoamini.


Mafanikio aliyopata
Pamoja na kwamba Tundu Lissu ni kijana aliyetoka katika maisha ya umaskini hivi sasa ni mbunge na mwanasheria, na mwanaharakati katika chama cha demokrasia na maendeleo, na nafasi hizo zimempatia kuishi maisha ya utajiri wa wastani akiwa na nyumba kadhaa pamoja na mali zingine zinazomtofautisha na mtanzania wa kawaida.
Pia amewezeza kupigania kile anachoamini hadi kufikia kuwa raisi wa Shirikisho la wanasheria nafasi ambayo iligubikwa na upinzani mkubwa. Hiyo inakupatia changamoto kubwa wewe ndugu msomaji kwamba kama Donald Trump alisimamia kile alichoamini na akapata kile alichotaka, pia Tundu Lissu amesimamia kile alichoamini na amepata kile alichotaka. Je wewe unasimamia nini? Upo tayari kufanya nini kwa ajili ya kile unachoamini kitakuwezesha kuinua biashara yako. Au ni nini kitakuwezesha kufikia malengo yako?
Mambo ya kuepuka
Ø  Epuka uchochezi
Ø  Epuka kutengeneza maadui wakubwa
Ø  Epuka kutokufuata sheria na kuipindisha pale inapoenda sawa na matakwa yako
Ø  Epuka hulka ya kuwa mgomvi kupindukia

Hitimisho
Nia kuu ya kuleta makala hii Kumhusu Mwanasheria Msomi Tundu Lissu ni ili kuleta kutafakari na kujifunza kutokana na safari aliyopitia. Lissu ni mfano bora kwa vijana kwamba haijalishi umetoka katika mazingira gani bado unaweza kufikia malengo yako ukitilia mkazo vipaumbele vyako. Kama mjasiriamali au mwajiriwa unapata mfano wa jinsi ya kusimamia kile unachoamini, kutilia mkazo katika vipaumbele katika kazi yako na mambo mengine ambayo unaweza ukayatafakari. Juu ya yote ili kufanikiwa ni lazima upitie hali ya changamoto nyingi, na unapimwa kulingana na unavyoruka viunzi katika kazi, masomo, biashara au maisha yako kwa ujumla.

Na Mkereketwa.

Comments

Popular Posts