kukata tamaa ni sumu itakayokufanya usifike pale unapotaka. ufanye nini?



Kukata tamaa
Ni hali ya mtu kukosa, kupoteza kitu au jambo na kutokua na matumaini kabisa ni kitu alichokipoteza. Hali hii huwatokea wajasiriamali pamoja wanafunzi vyuoni na wafanyakazi wengi tena mara nyingi sana, lakini sasa nini nini tunachopaswa kufanya kama wajasiriamali, wafanya biashara ambao mtaji umeisha, madeni yameongezeka, au labda ni wafanyakazi ambao hatujaridhika na majukumu tunayofanya au wanafunzi ambao hawana uhakika na kumaliza chuo, kupata kazi au kusimamisha mradi fulani. Ungana nami…
Kwanini watu hukata tamaa?

1. Kuishi maisha ya kuigiza;
Kuishi maisha ambayo siyo yako kwanza ni utumwa unaanza kulinganisha maisha yako na mtu mwingine, unaanza kujilinganisha na jirani yako yeye ana kitu fulani na wewe huna, unaanza kuwa na matumizi yasiyo muhimu ili mradi tu ufanane na Fulani, hii hupelekea akiba kuisha, mtaji kupotea na wanaokudai iwe ni benki au vicoba, taasisi za kukopesha au watu binafsi waliokukopesha wanapokuandama kukupatia msongo utakaokufanya ukate tamaa na kufikiria kuacha unachofanya. Ishi maisha yako na usijifananishe na mtu mwingine. Waswahili wanasema iga kazi usiige matumizi. 2. Kuzungukwa na watu hasi;

Kuzungukwa na watu wenye mtazamo hasi nayo ni changamoto inayosababisha watu wengi kukata tama. Watu wenye mtazamo hasi kazi yao ni kukosoa utafikiri wako katika mashindano ya kukosoa, na katika kukosoa wanakosoa kwenye jambo zuri au baya ili afanikishe tu kukujaza fikra hasi kama alizokuwa nazo.
Ukiwa na mawazo mazuri usimshirikishe mtu wa namna hii, tafuta mtu chanya awe mshauri wako, pendelea kujifunza sana, soma vitabu, makala, hudhuria semina hakika utakua umezungukwa na watu wenye fikra chanya. Epuka kuzungukwa na watu wenye mtazamo hasi, na zungukwa na watu wenye mtazamo chanya itakuepusha na kufikiria kukata tama. Haupaswi kukata tamaa kabisa kwani ni dhambi endelea kuweka juhudi na maarifa na pambana mpaka utakua mshindi.
3. Kuandamwa na mikopo
Watu wengi wamejiingiza katika mikopo isiyo na faida na mikopo hiyo imekuwa sababu kubwa ya kufilisika kwa watu wengi lakini pia mikopo imekuwa daraja la kupafanikiwa katika biashara kwa baadhi ya wajasiriamali, vijana wa chuo wanaopokea mkopo na kuutumia vyema, na hata wafanyakazi waliowekeza kupitia mikopo. Nitazungumza kwa undani kuhusu mikopo katika makala zitakazofuata.
4. Maamuzi mabaya
Baadhi ya watu huwa na uwezo wa kutafuta fedha na kuzipata ili tu kuzipoteza kutokana na maamuzi mabaya katika biashara. Labda ulimwamini sana mtu ambaye hukupaswa kumuamini, au ulisaini mkataba ambao hukupaswa kusaini, kufanya manunuzi mabaya, na hata kutoa maamuzi ya mwelekeo wa biashara yasiyokuwa ya hekima.


Mifano ya waliokata tamaa

1. Al Bubba ni mjasiriamali anayeendesha migahawa na uzalishaji wa bidhaa kadhaa nchini Marekani. Alipata ujuzi wa kuchoma mbavu za ng’ombe kwa staili ya tofauti kutoka kwa baba yake. Na aliufanyia kazi ujuzi huo lakini kwa wakati ule biashara ilikuwa ngumu na akakata tamaa, lakini miaka ishirini baadae binti yake ambaye ndio alikuwa amezaliwa tu wakati wazo hilo lilipoanzishwa, yeye ndie aliyemshawishi kurudi katika biashara hiyo na sasa anatengeneza mamilioni ya pesa kwa “Kuchoma nyama”

2. Agustine Mrema alikuwa mwanasiasa machachari miaka ya tisini hadi kufikia hatua ya kugombea urais mara kadhaa, lakini alikata tamaa ya kuufukuza urais bila mafanikio na akaamua kuwa mbunge.

3. Kanali Harland David Sanders wa KFC, kampuni kubwa ya migahawa chakula ambayo imejikita hasa katika mapishi ya kuku, ni kampuni yenye jina kubwa duniani na maelfu ya migahawa duniani. Lakini kanali huyu akiwa na umri takribani miaka sitini alikuwa amekata tamaa ya maisha na alitaka kujiua lakini alipokuwa akiandika barua yake ya mwisho alitafakari kwa makini na kujiuliza kama ametumia ipasavyo kipaji chake, akaona bado hajaweka jitihada zake za mwisho na hatimaye alienda kuchukua pesa za msaada kutoka serikalini na akaanza mradi wa kuukaanga kuku na kuwauza milangoni mwa watu, hatimaye kufikia alipo sasa.

Kwanini usikate tamaa
Mungu ametupatia pumzi kila mmoja wetu, wote tumepatiwa masaa ishirini na nne, siku saba na wiki hamsini na mbili kila mwaka wa maisha yetu. Kwanini ukate tamaa wakati bado unapumua na fursa nyingi zinakuzunguka katika maisha yako. Hakuna sababu ya kumfanya mtu akate tamaa. Kwa sababu unaweza kushinda hicho kinachokukatisha tamaa.
Ufanye nini unapohisi kukata tama
1. Tafuta chanzo (Usijidanganye wala Usijilaumu):  
Kulalamika, kujilaumu hakusaidii kutatua tatizo linalokukabili, au hilo jambo  linalokukwaza. Badala yake tafakari kwa umakini na kwakuwa mkweli wa nafsi yako ili kujua kwanini hasa tatizo biashara au kazi yako imekukwamisha au haiendi ulivyokuwa unataka na imekukatisha tamaa, na huo utakua mwanzo mzuri wa kujifunza kutokana na makosa badala ya kukata tamaa.


2. Tengeneza picha kubwa ya maisha: 
Kwa sehemu kubwa wanaokata tamaa katika biashara Fulani ni kwa sababu uwezo wao wa kufikiri umeishia hapo katika hicho kilichomkatisha tamaa, na hawezi kukaa na kufikiria kwamba sio mwisho wa safari ya ujasiriamali. Beatrice alikua ana duka la vipodozi, lakini kuna siku alitembelewa na maofisa wa TRA na bahati mbaya hakuwa na leseni na ilimbidi kuhonga laki mbili, bahati mbaya zaidi alikuwa na hali mbaya ya kiuchumi na fedha ile alishindwa kuirejesha mahali pake, kila alichouza alipeleka kwenye matibabu ya mdogo wake aliyekuwa na matatizo ya kifafa na mwisho wake duka likafilisika, anadaiwa laki tano pamoja na kodi ya fremu laki nne na themanini na alikua hajui afanye nini. Leo ana leta nguo na viatu kutoka uturuki, na hongkong. Kwa nini, ni kwasababu mawazo yake hayakuishia kuuza vipodozi, alihangaika kufanya kibarua katika duka la rafiki yake na hatimaye akamaliza deni, kuku wake wakawa wako tayari kwa soko akapata mtaji wa kusafiri. Fursa moja inapokwisha, rekebisha makosa, anza upya ukiwa umejifunza, lakini kwa mara hii ufanye kwa upeo mpana maana umefuzu shule hiyo. Kama mjasiriamali unapaswa kuwaza mbali kwa upeo mpana.

3. Nafasi yako katika kuleta matumaini ya maisha: 
Pamoja na kuwa unahitaji watu wengine kukupa msaada na kushirikiana nao katika mambo kadhaa , wewe kama wewe una nafasi kubwa zaidi ya hao wote ukiwajumlisha. Mfano katika hali hiyo ya kukata tamaa, wewe ndie pekee mwenye uwezo wa kuamua kuwa sasa kukata tamaa basi, na badala yake utafute suluhu ya hilo linalokuumiza, na kama suluhu haiji haraka basi ni bora kulipuuzia jambo husika, kwani kama hauwezi jambo usiloweza kulipatia ufumbuzi , hata ukihuzunika, haisaidii kwani wakati huu unapokuwa umekata tamaa, jambo kubwa unalolihitaji ni ufumbuzi wa hilo tatizo. Hivyo kama ufumbuzi wa tatizo haupo kwa mujibu wa ufahamu wako, basi ni bora kuangalia njia nyingine kuliko kuendelea kuhuzunika.

4. Usijilinganishe:   
kujilinganisha na watu wengi kunaweza kuchochea kukata tamaa zaidi kwani siku zote wapo watu waliofanikiwa zaidi  na uwezo au nafasi kubwa kuliko wewe katika sekta uliyoshindwa.
Kumbuka kukata kwako tamaa ni jambo lako binafsi hivyo inabidi utafute ufumbuzi binafsi na sio kujidimiza kwa kujilinganisha na wanaoendelea kufanikiwa, jambo bora ni kwenda na kujifunza kutoka kwao, usijitenge nao kwa sababu unajiona wa chini kwa sababu ya biashara yako.
Isitoshe maisha ni safari ndefu , hao unaodhani walio bora pengine siku si chache watakuwa wapo chini kibiashara kuliko ulivyo wewe.

5. Hali ngumu = Fursa ya kuwa bora zaidi: 
Kuna msemo unaosema akili ya mtu hufanya kazi zaidi pale anapokua na njaa. Yaani hali inapokua ngumu ndipo macho yako huziona fursa. Robert Kiyosaki alipanda katika utajiri kutoka kwenye kuishi ndani ya gari lake. Erick Shigongo alifanikiwa kutoka kwenye umaskini wa kwao na hivyo hali ngumu haipaswi kukufanya ukate tamaa lakini fungua akili yako na utaziona fursa zikiwa zimekuzunguka.

6. Kumbuka uwezo wako na sio mapungufu yako:   
Unajpojisikia  kukata tama katika biashara yako au kazi yako, kumbuka wewe mwenywe ndio ndio msaada mkubwa katika kukabiliana na hali hiyo, na njia kubwa zaidi ya kufanikiwa ni kukumbuka mambo makubwa unayoweza kufanya, na sio madhaifu yako. Tafakari ni jinsi gani umefanya mambo chanya katika jambo linalokukatisha tamaa na mambo hayo yakusukume kufanya vyema zaidi.

7. Kumbuka fadhila na mafanikio:   
Watu watakao kusaidia katika kukata kwako tamaa ni wale uliowafadhili au uliowasaidia kufanikiwa hivyo wekeza kwa watu ukingali bado una kitu na kama hukufanya hivyo anza leo. Yule omba omba, mtoto wa jirani yako aliyeko nyumbani kwa kukosa ada, Yule mwanafunzi wa chuo ambaye hana mkopo, Yule ambaye biashara yake imekwama, anzia popote, anza na wale walio karibu nawe
Zungumza/Omba msaada:
Usikae kimya na hali yako  inayokukatisha tamaa. Tafuta msaada kwa watu sahihi. Jitahidi kutambua aina sahihi ya watu wa kuwa nao karibu hasa unapokuwa katika hali ngumu ya kukata tamaa kwani baadhi ya watu watakuongezea kukata tamaa. Lakini pia kumbuka anayetoa au anayetwaa kile ulicho nacho ni Mungu hivyo muombe mungu wako akuwezeshe kuvuka hapo ulipo

Hitimisho
Kukata tamaa ni sumu ya mafanikio ya kila mtu, katika kila jambo unalofanya litazame kama ni sehemu ya ngazi ya kukufikisha unapotaka, inapokatika haurudi chini na kuanza kuumia, unatafuta njia nyingine ya kufika pale unapopataka kwa kujifunza kutokana na kilichokukatisha tamaa.


Comments

Popular Posts