SASA HIVI NDIO WAKATI WAKO WA KUWA MJASIRIAMALI



Ni wakati wa kuwa mjasiriamali
1. Anza hapo ulipo leo.
Ujasiriamali sio tu kuhusu kutengeneza fedha, lakini ujasiriamali ni mtazamo, ni mtindo wa maisha yani mjasirimali ni Yule mtu anayetamani kuona badiliko na anafanya kitu kwa ajili ya kuleta badiliko hilo kwa njia ya kuvumbua kitu, kuboresha kitu Fulani ambacho kilishakuwepo lakini hakikidhi matakwa ya badiliko hilo lakini kwa namna iliyo endelevu.
Unaweza ukawa ni mtu asiye kuwa na ajira, au labda umeajiriwa lakini una mawazo ya kuwa mjasiriamali, au labda upo chuoni au umemaliza chuo lakini ajira hakuna. Jambo la kwanza anza hapo ulipo, nikuambie tu kwamba Mungu ameweka fursa kwa ajili ya kila mwanadamu lakini ni wajibu wako kuweza kutambua fursa hiyo ili uweze kuitumia kwa manufaa yako.
jambo kubwa la kwanza ni kuwa mahali sahihi, kwa wakati sahihi. unapokuwa mahali sahihi na mtu sahihi, kwa wakati sahihi basi unauwezo mkubwa wa kuona fursa ikipita na ni wajibu wako kuweza kuchukua fursa hiyo. Ile hali ya kuishi hapo ulipo ni fursa kwa sababu hakuna mahali walipo wanadamu pasipokuwa na matatizo, ni kazi yako kutatua matatizo hayo na kutengeneza pesa wakati ukifanya hivyo, mangi wa dukani pale unapoishi aliona tatizo kwamba watu hawa wanamahitaji ambayo nikienda mahali Fulani kuwaletea hapa karibu wanaweza kununua, na hadi kesho mangi anawauzia mahitaji yenu, mama lishe aliona tatizo la chakula, Fulani aliona tatizo la maji. Manji aliona tatizo la kuni na mkaa akaleta Manjis gas, Gwajima aliona tatizo la watu kuhitaji miujiza akafungua kanisa na wote hawa kwa kutatua tatizo Fulani walikuwa wajasiriamali wakubwa.



Nitakupatia mfano mmoja kwa undani.

Patrick Ngowi aliona tatizo la umeme akaleta sola. Patrick alipokuwa na miaka 15 alianza kwa kuona hitaji la vocha kwa wanafunzi wenzake na akaanza kuwauzia vocha na kwa mtazamo au hali ya akili aliyokuwa nayo wakati huo hakuishia kuuza vocha kwa wanafunzi wake lakini aliongezeka na kufahamika kwa sababu maeneo ya hapo kulikuwa na uhaba wa vocha. Hadi kufikisha umri wa miaka 18 alikuwa ni mjasiriamali anayeuza simu kutoka nje, baada ya kuonyesha nia na juhudi katika kile alichokuwa anakifanya mama yake alimkopesha takribani milioni mbili na rafiki yake mmoja akamlipia tiketi ya ndege na akaenda China kuleta simu kwa mara ya kwanza. Na kutokana na uhaba wa simu wakati huo biashara yake ilikuwa kubwa. Alianza na kile alichokuwa nacho, alianza na hitaji lililokuwa karibu, aliuza vocha, na kama wewe ni mjasiriamali kutoka kwenye damu basi utaendelea kutatua matatizo jinsi unavyokua na kuendelea kupata mafanikio.
Pamoja na yote, ujasiriamali pia ni safari, unaanza taratibu mahali ulipo na unaendelea na kukua katika changamoto utakazo kutana nazo kwa sababu umejitoa kutatua matatizo usishangae matatizo pia yakiongezeka, pale ambapo kuna changamoto ndipo penye fursa na fursa yenyewe inaweza ikawa kujifunza kutokana na kile kilichokupatia changamoto.



Sehemu ya pili ya makala hii:
2. Usikate tamaa, kwa nini usikate tamaa na ufanye nini unapokata tamaa.


Comments

Popular Posts