Paul Makonda/ Bashite umejifunza nini?



Mambo ya kujifunza katika maisha ya Makonda/Bashite
Maisha yamejaa mafundisho katika kila kitu kwa aliye tayari kujifunza. Wenye hekima walisema somo utakalojifunza kutokana na kushindwa jambo ni bora kuliko lile utakalosoma bila kulifanyia kazi na kushindwa au kufaulu. Lakini pia ningependa kuongeza maneno yangu mwenyewe kwamba ni bora kujifunza kutokana na makosa ya mtu mwingine na kufanikiwa. Nakumbuka niliwahi kufanya mradi Fulani miaka mitatu iliyopita na nikashindwa ila rafiki yangu mmoja akarekebisha makosa yangu nay eye akaufanya mradi ule kwa mafanikio. Hivyo tunaweza kujifunza jambo kutokana na maisha ya Paul Makonda/Bashite kwa kuchuja mazuri na mabaya.
Kwanza tuanze kwenye msingi wa maisha yake. Makonda hakuzaliwa Dar ni “mwanaume wa mkoani” kama ulivyo msemo wa wadaslam wengi (borntown), alizaliwa Mwanza wilaya ya Misungwi, kijiji ha kolomije tarehe 15 Februari. 1982, akiwa ametokea kwenye familia maskini akiwa mtoto pekee (kuna madai kwamba aliwahi kuwa na ndugu wa kike akafariki).
1. Umaskini: Paul Makonda alitokea katika familia ya kimaskini katika kijiji cha mbali akiwa na baba ambae hakusoma na mama wa darasa la saba, lakini hiyo haijamzuia kuwa mkuu wa mkoa na kutikisa nchi. Wengi wamekuwa wakisema kwamba labda ningezaliwa kwenye hali bora kidogo ningeweza ku… labda nyingi. Lakini pia umaskini ni mwalimu bora wa mafanikio kwa Yule aliyetayari kujifunza na kufanya kazi kwa bidii.
Paul Makonda amesoma shule nyingi sana wengi husema kwa sababu alikuwa kilaza lakini huenda umaskini wa wazazi wake ulichangia pia, anayefahamu ni yeye. Alisoma Kolomije shule ya msingi, na alipomaliza kidato cha nne alienda kusomea uvuvi ngazi ya cheti huko Bagamoyo lakini hakuishia hapo aliungaunga diploma na hata kufikia kusomea shahada yake ya kwanza.
2. Vikwazo katika Elimu sio mwisho wa maisha: wengi sasa wanamuita Makonda/Bashite kuwa kilaza baada ya kusemekana kutumia cheti cha mtu. Lakini ifahamike kwamba wakati Makonda anakua Elimu ilikuwa ndio ufunguo wa maisha na yeyote ambaye hakusoma alisota sana, na ufahamu juu ya hilo ukamfanya Makonda aone haja ya kuendelea kusoma japo hakukidhi vigezo. Jambo la kujifunza hapa ni kwamba hata kama umetoka katika familia maskini, au huna elimu yoyote bado unaweza ukawasumbua sana wakuu wa mji. Unachopaswa kufanya ni kuweka mkazo katika vipaumbele vyako na kuwa na bidii katika kufikia malengo yako. Kwa makonda lengo lake kuu ilikuwa ni kuukimbia umaskini, na hiyo inatuleta kwenye jambo lingine;
3. Uchapakazi: inasemekana kwamba Paul Makonda/Bashite alikuwa ni mchapakazi sana, aliwahi kuwa konda wa mabasi, aliwahi kuwa mchimba mchanga, mkata kokoto nk. Kazi ambazo alizifanya kwa bidii akitaka kuyafikia malengo yake. Sasa sikuambii uende ukawe konda wa mabasi lakini ninataka kukuonyesha kwamba kila alichoshika alifanya kwa bidii hata alipokuwa chuoni na vyeti feki kwa bidii yake aliweza kuwa waziri mkuu wa serikali ya wanafunzi, hivyo kila ulifanyalo kwa mkono wako au kwa akili yako fanya kwa bidii, mafanikio hayapo katika uvivu na kupenda starehe.
4. Kazi yako izae matunda: akiwa mkuu wa wilaya aliwapigania waalimu waweze kusafiri bure, aliweka mikakati ya kukabiliana na ajira, alishiriki kushawishi watu kusalimisha silaha, alikamata tani 4 za sukari wakati wa sakata la sukari, alipambana na omba omba, alitumbua watumishi hewa nk.
Kila unachopata nafasi ya kufanya kifanye kwa bidii kizae matunda nawewe utaonekana na wakubwa zako.
Baada ya kuona mambo chanya kutoka kwa mkuu wa mkoa ni vyema kupitia mambo hasi ambayo ni bora kujifunza kuyaepuka;
1. Majivuno: kama ilivyo kawaida kwamba masikini anapopata huwa anataka kila mtu ajue kwamba amepata, Bwana Bashite ametoka katika familia ya kimaskini amepambana hadi kufika alipo leo, lakini kama wahenga walivyozema kwamba “kiburi hutangulia uangamivu”. Kutokana na majivuno ya utajiri wake mali zake zimekuwa gumzo hadi bungeni hali inayotia mashaka uhalali wake ambapo kama yangekuwa maisha yake binafsi huenda angekuwa na matatizo kidogo leo. Hatupaswi kuwa watu wa kuonyesha kile tulicho nacho sana, japo ni ngumu kwa watanzania ila unaweza ukajifunza kitu hapa.
2. Kulewa Madaraka: wengi wetu tumekuwa Makonda huko maofisini kwetu au tumekutana na mabosi walio kama makonda na hii inakufanya upoteze rasilimali watu, yaani watu watakaokuwa nawe watakuwa nawewe kwa sababu wanakuogopa tu sio kwa sababu wanakuheshimu, hii inafaa hata mashuleni kwa wanafunzi wanaotaka au walio katika uongozi, maofisini- jinsi ya kuwa bosi ambaye hata ikitokea kashfa wafanya kazi wako watakuwa tayari kusimama na kukutetea, na sio kusema “atatumbuliwa lini huyu naye”
3. Dharau: taarifa kutoka kwa wafanyakazi wa karibu wa Makonda wanasema ni mtu mwenye dharau nyingi sana kwa wafanyakazi wake na watu wengine, mfano aliwahi kumuaibisha mtumishi wa ngazi ya juu mbele ya mkutano mzima akimtaka afanye lile alilokuwa anataka yeye. Unapokuwa na hali hii watu husubiri kwa hamu anguko lako, hata kama una mali nyingi kiasi gani, heshima na hekima, au una cheo gani, ubora wa utu wako utapimwa kwa jinsi unavyowatendea watu wengine.
Wote tuna bisi zetu mikononi tunakula taratibu kuona jinsi mwisho wa sakata la Makonda litakavyokuwa, lakini kwa mtu mwenye hekima atajifunza kitu katika maisha ya mtu huyu na kuepuka kurudia makosa katika sehemu zetu za kazi. Lakini pia wewe kijana unayesoma makala hii utakuwa umeona wazi kwamba hakuna kinachokuzuia kufikia malengo yako. Kama kijana kutoka katika familia ya kimaskini huko Mwanza kijiji gani sijui ameweza kuwa mkuu wa mkoa. Wewe kijana wa hapa Dar unaweza hata kuwa mwenyekiti wa Afrika Mashariki ukiweka nia, juhudi, na uvumilivu katika malengo yako.
Imeandaliwa na mkereketwa wa mtandao
MM.


Comments

Popular Posts